Brazil yakataa Msaada wa G7 Kuzima moto msitu wa Amazon

Brazil yayashutumu mataifa tajiri ya G7 kutaka kuupoka msitu wa Amazon

A handout photo from Greenpeace Brazil showing smoke rising from the fire at the Amazon forest on 23 August 2019Haki miliki ya pichaEPA
Serikali ya Brazil imetangaza kususia msaada wa fedha kutoka nchi za G7 zinazolenga kupambana na moto wa nyika katika msitu wa Amazon.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron - ambaye aliandaa mkutano wa G7 uliofikia tamati Jumatatu - amesema kiasi cha dola milioni 22 kitatolewa.
Lakini mawaziri wa Brazil wanasema fedha hizo hazihitajiki na kuwashutumu mataifa hayo yenye nguvu kwa kutaka kuutawala msitu wa Amazon.
Picha za satalaiti zinaonesha kuwa msitu huo mkubwa zaidi duniani unateketea kwa kasi inayovunja rekodi.
Amazon inaangaliwa kimataifa kwa kuwa asilimia 20 ya hewa safi duniani kote inazalishwa kwenye msitu huo.
Katibu Mkuu wa Rais wa Brazil Onyx Lorenzoni, ameuambia mtandao wa habari wa Globo kuwa: "Asante, lakini fedha hizo yawezekana ni muhimu kwa kuhuisha misitu ya Ulaya.
"Macron hawezi hata kuzuia moto uliotarajiwa kwenye kanisa ambalo ni la urithi wa dunia, kisha anataka kutupa funzo kuhusu nchi yetu wenyewe? Bw Lorenzoni ameongeza, akimaanisha moto ambao ulilikumba kanisa la Notre-Dame mwezi Aprili.
Waziri wa Mambo ya Nje Ernesto Araujo amesema kuwa tayari kuna njia za kupambana na moto huo chini ya Umoja wa Mataifa (UN).
"Jitihada za baadhi ya mataifa kushadadia masuala ya kimazingira na kuyafanya kuwa 'majanga' ili kuzaa mbinu za kuutawala msitu wa Amazon kutoka nje zinaonekana dhahiri,"ameongeza kwa kupitia ujumbe wa Twitter.
Awali rais wa Brazil, Joao Bolsonaro alisema kuwa serikali yake haina fedha za kutosha kupambana na moto huo.
Baadhi ya wanaharakati wanasema hata fedha zilizoahidiwa na G7 kuwa ni kiduchu kulinganisha na ukubwa wa janga linaloendelea.
Jana Jumatatu, mwuigizaji maarufu, Leonardo DiCaprio aliahidi kutoa dola milioni 5 kwa ajili ya kusaidia kuzima moto huo.
Dola milioni 22 zilizoahidiwa zinatoka mataifa ya - Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japani, Uingereza na Marekani.
Rais Macron amesema pesa hizo zitatolewa haraka iwezekanavyo - ili ziweze kulipia ndege zaidi za zimamoto - na pia Ufaransa itatoa msaada kwa jeshi la Brazil.

Kwa nini umezuka utata?

Image captionMaandamano nchini Brazil yanaendelea yakitaka usaidizi wa kimataifa
Bolsonaro amekuwa akimshutumu vikali Macron kwa kujifisha nyuma ya umoja wa G7 kufanikisha malengo yake ya kibeberu ya kutaka kupoka hatma na ustawi wa Amazon kutoka kwa wananchi wa Brazil.
Kwa muda mrefu kiongozi huyo amekuwa akizituhumu nchi za Ulaya zimekuwa zikijaribu kujipenyeza na kuchota rasilimali za Brazil.
Mwezi Julai aliwaambia waandishi wa habari kuwa: "Brazil ni kama msichana bikira ambaye walaghai wote kutoka nje wanamnyemelea."
Pia amedai kuwa mataifa ya Ulaya "yanaamini vichwani mwao" kuwa Amazon haimilikiwi na Brazil.
"Nchi hizi zinazotuletea pesa, hazifanyi hivyo kwa nia ya kutusaidia," amesisitiza wiki iliyopita na kuongeza, "Wanafanya kwa malengo ya kuingilia uhuru wetu."
Hata hivyo, safari huu kumekuwa na shinikizo kubwa kwa viongozi wa Brazil juu ya moto unaoendelea.
Brazil inasema wanajeshi 44,000 wapo mstari wa mbele kuuzima moto huo katika majimbo saba.

Post a Comment

0 Comments