Mr Puaz: Meneja wa zamani wa Harmonize asema msanii huyo ataimarika zaidi nje ya WCB

Mr Puaz na Harmonize

Haki miliki ya pichaMR. PUAZ
Msanii wa muziki wa Bongo Fleva ambaye yupo katika harakati ya kuondoka katiika kundi la Wasafi nchini Tanzania Harmonize ana uwezo wa kupiga hatua kubwa iwapo atajiondoa katika WCB.
Hayo ni kwa mujibu wa meneja wa zamani wa msanii huyo Joel Vincent maarufu kwa jina Mr. Puaz aliyesema kwamba msanii huyo ana uwezo wa kupanua mbawa zake na kuwa zaidi ya msanii pekee chini ya kundi lake.
Bwana Puaz ambaye alitengana na msanii huyo kutokana na tofauti zao za kibinafsi anasema kwamba ni vigumu kwa Harmonize kushamiri chini ya WCB kwa kuwa kuna sheria ambazo zinamzuia kujiendeleza ama hata kufanya maamuzi.
''Unajua unapokuwa chini ya makubaliano fulani kuna sheria ambazo zitakufinya kidogo katika kona ambapo unakua huwezi kufanya mambo zaidi ama hata kuafanya uamuzi'', alisema bwana Puaz katika mahojiano na mwandishi wetu.
''Naamini kwamba iwapo ana mipango mizuri baada ya kuondoka ataimarika zaidi kutokana jina lake kubwa katika soko'', aliongezea.
Kulingana na meneja huyo wawili hao - Harmonize na Mr. Puaz -waliamua kutengana kutokana na kile alichokitaja kuwa ukosefu wa maelewano katika biashara hiyo.
Mr Puaz ambaye alizungumza na BBCSwahili kwa njia ya simu alisema kuwa Harmonize alikuwa akimdharau na kupuuza ushauri wake.
Hatahivyo kulingana na Mr. Puaz wawili hao wamesuluhisha tofauti zao na sasa ni marafiki
Afisa mtendaji wa kundi la WCB Sallam SK maarufu Mendez, amesema kwamba Harmonize tayari ameandika rasmi kwa kundi hilo akisema anataka kujiondoa.
Sallam amesema kwamba kwa sasa moyo wa msanii huyo haupo tena na WCB na ameitisha mkutano na usimamizi wa WCB katika harakati yake ya kukubaliana na hatua hiyo.
"Harmonize kwa sasa moyo wake haupo WCB, kimkataba bado yupo. Kwa nini nasema hivo? Harmonize ameshatuma barua ya maombi ya kuvunja mkataba na yuko tayari kupitia vipengele vyote vya sheria kusitisha mkataba wake na ni kitu ambacho tumependezewa nacho. Yeye mwenyewe ameridhia na ameomba kikao na uongozi," alisema Sallam.
Sallam alisema kwamba kwa sasa kundi la mahasibu litafanya hesabu zao kuamua iwapo msanii huyo alipata faida ama hasara katika WCB.
Kulingana na usimamizi wa WCB Harmonize baadaye atakabidhiwa faida yake yote ama kulazimishwa kulipa hasara aliopata.
Lakini akizungumza na BBCswahili Puaz alisema kwamba Harmonize ni mtu mchapa kazi na mwenye bidii hivyobasi iwapo atakuwa na mikakati mizuri na washirika wazuri atafanikiwa pakubwa katika siku za usoni.
Aliongezea kwamba kiongozi wa WCB Diamond Platinumz hafai kulinganishwa na msanii yeyote wa WCB kwa kuwa atasalia kuwa mtu aliyebadilisha maisha ya Harmonize na wengine wote katika kundi hilo.
'' Nadhani hatoki WCB ili kushindana na Diamond bali anataka mapato mazuri zaidi ya anavyopata kwa sasa, hivyobasi lazima atoke nje . Hata mtoto mdogo akishakua na kuona kwamba sasa anafaa kuwa na familia yake ataondoka nyumbani kwao''.
Alisema kwamba, msanii huyo atalazimika kuteua kikosi cha wataalam wenye uzoefu katika maswala ya mawasiliano na uongozi ili kumsaidia mwimbaji huyo wa wimbo 'my boo' kushamiri katika azma yake mpya
''Iwapo ataweza kusimamia vizuri mawasiliano yake na uongozi bila shaka atakua msanii mkubwa sio tu Afrika bali pia duniani''.
''Natumai amejifunza mengi kutoka kwa Diamond hivyobasi hatafanya makosa aliyoyaona katika kipindi chake chote na WCB'', aliongezea.
Tulipomuuliza iwapo yuko tayari kushirikiana na msanii huyo katika kundi lake jipya iwapo ataondoka WCB, Bwana Puaz ambaye kwa sasa anawasaidia wasanii chipukizi nchini Tanzania kuafikia ndoto zao alisema: Mimi na yeye tumemaliza tofauti zetu na sasa sisi ni marafiki lakini ndio ningependa kushirikiana naye nimsaidie pale nitakapoweza.
Harmonize atalazimika kuwasili mbele ya bodi ya WCB kuelezea kwa nini anataka kujiondoa katika kundi hilo kabla ya kandarasi yake kufutwa.

'Kwangwaru '

Wakati huohuo wimbo ulioimbwa na Diamond akishirikikana na Harmonize 'Kwangwaru' umeweka historia baada ya kuwa kibao cha kwanza cha Tanzania kilichotazamwa mara milioni 50 katika mtandao wa Youtube.
Wakati kibao hicho kilipotolewa kilivutia ushabiki mkubwa Afrika mashariki na kuorodhesha cha kwanza katika redio na runinga kadhaa.
Akitoa tangazo hilo katika ukurasa wake wa instagram Harmonize alimpongeza sana Diamond Platinumz.
Aliandika: Wow.. milioni 50 Mungu ni mzuri...pongeza maalum zinakwenda kwake ndugu yangu mkubwa #SIMBA @DiamondPlatinumz, tulishirikiana pamoja kuzalisha wimbo huu , tuonane ,msanii huyo aliandika.

Post a Comment

0 Comments