tangazo

Watoa tamko la kumpongeza Rais Magufuli


Baraza la Jumuiya ya Wazazi CCM wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga limetoa tamko la kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Tamko hilo limetolewa jana wakati wa kikao cha kawaida cha Baraza la Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Kahama kilichofanyika katika kijiji cha Magung’humwa kata ya Mwakata wilayani Kahama.

Akisoma tamko hilo, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi (CCM) wilaya ya Kahama, Disco Wabare amesema kuchaguliwa kwa rais Magufuli kuongoza SADC inaonesha dhahiri imani waliyonayo viongozi wa SADC kutokana na umahiri na utendaji kazi wake kwa wananchi wa Tanzania na Jumuiya ya SADC.

“Kwa heshima na unyenyekevu mkubwa baraza la Wazazi la wilaya ya Kahama kwa pamoja tunatoa tamko la kumpongeza Rais wetu mpendwa,mwenyekiti wa CCM taifa,Amiri Jeshi Mkuu na mtetea wanyonge, Mhe. John Pombe Magufuli kuwa mwenyekiti mpya wa SADC”,amesema.

“Sisi kama Baraza la Wazazi Kahama tunategemea kuona mabadiliko makubwa katika uongozi wake hasa katika kukuza uchumi wa nchi za SADC na kuondoa tatizo la ajira ambalo limekuwa kikwazo kikubwa kwa vijana wa nchi hizo”,ameongeza Wabare.

Amebainisha kuwa Baraza la wazazi Kahama linaamini kuwa kwa kasi aliyonayo Magufuli katika kuendeleza nchi ya Tanzania kimaendeleo,ataitumia pia katika kuendeleza umoja wa SADC kwa kipindi cha mwaka mmoja aliochaguliwa kuongoza SADC.

Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM mkoa wa Shinyanga,Salim Abdalah Simba alisema pamoja na kumpongeza Rais Magufuli ni vyema WanaCCM na Watanzania kwa ujumla kumuunga mkono kwa kufanya kazi kwa bidii.

Post a Comment

0 Comments