Dkt. Ndugulile ataka maboresho ya mifumo ya takwimu



Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile ametaka maboresho ya mifumo ya takwimu za tafiti mbalimbali zinazofanyika nchini.

Dkt. Ndugulile amesema hayo wakati akizindua kongamano linalohusisha wadau mbalimbali wa masuala ya UKIMWI ambao wanawasilisha tafiti na takwimu mbalimbali ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi nchini.

“Tunahitaji tuboreshe mifumo yetu ya takwimu ili tuwe na uwiano wa takwimu ambazo zinawasilishwa katika mkutano huu, hapa nimeona takwimu mbalimbali zimewasilishwa, ninaomba takwimu hizo ziwe za wote kwa sababu tuna wadau wengi wanaoshiriki katika mapambano haya dhidi ya Ugonjwa wa UKIMWI hivyo maelekezo yangu kuwe na mfumo mmoja wa takwimu ambao kila mmoja atakua anachangia takwimu zake na mfumo huo uwe wa mwisho utakaotoa takwimu za wote”. Amesema Dkt. Ndugulile.

Hata hivyo Dkt. Ndugulile amehamashisha makongamano kama hayo yafanyike mara kwa mara ili kuwawezesha wanazuoni, watunga sera na walengwa kukaa pamoja ili kujadiliana mambo mbalimbali ambayo yanahusuana na afua ambazo zinatekelezwa hapa nchini.

Kongamano hilo limeshirikisha taasisi za Serikali ambazo ni NIMR na TACAIDS pamoja na wadau mbalimbali wanaofanya tafiti kuhusiana na ugonjwa wa UKIMWI ambao wamekutana ili kuwasilisha takwimu za tafiti mbalimbali ambazo wanazifanyia kazi katika maeneo yao.



Post a Comment

0 Comments