tangazo

Serikali yatoa Tsh. Bilion 30 kwa ajili ya huduma za Chanjo

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto yatoa kiasi cha shilingi Bilion 30 kila mwaka kwaajili ya huduma za Chanjo ili kuwakinga wananchi dhidi ya magonjwa mbali mbali.

Hayo yamesemwa na waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu jana wakati akikabidhi magari 71 ya chanjo kwaajili ya Halmashauri 61, na magari 10 kwaajili ya Mpango wa chanjo nchini ikiwa ni sehemu ya kuimarisha huduma za chanjo kwa Wananchi.

Waziri Ummy amesema kuwa, Serikali imetoa magari hayo ili kurahisisha shughuli za chanjo katika maeneo mbali mbali hivyo, ameagiza magari hayo yakafanye kazi kulingana na madhumuni yaliyokusudiwa.

Aliendelea kusema, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa Halmashauri zote zilizobaki zinapata magari ya chanjo ili kurahisisha utendaji kazi katika maeneo yote nchini.

Kwa upande mwingine Waziri Ummy amesema kuwa, Serikali imetoa na kusambaza majokofu zaidi ya 1300 yanayotumia umeme wa sola katika Halmashauri zote nchini, jambo lililosaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa majokofu hayo.

Mbali na hayo, Waziri Ummy ametoa wito kwa wazazi na walezi wote nchini kuhakikisha wanawapeleka Watoto katika vituo vya kutolea huduma za Afya kupata chanjo ili kuwakinga dhidi ya magonjwa ya surau na lubena.

Hata hivyo, Waziri Ummy amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya wote nchini kuhakikisha wanawafikia Watoto wote nchini walio na umri wa chini ya miaka mitano, kuwapa huduma za chanjo ili kuwakinga dhidi ya magonjwa.

Post a Comment

0 Comments