Tundu Lisu aahirisha tarehe ya kurudi Tanzania


Tundu Lissu
Image captionTundu Lissu anasema bado ana nia ya kugombea urais
Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu, amesema sio bayana kwamba atarudi nyumbani Tanzania tarehe 7 Septemba.
Tarehe hiyo Septemba 7 ni miaka miwili tangu Lissu kushambuliwa na watu wasiojulikana.
Katika kipindi cha nyuma mwanasiasa huyo alidokeza kuwa atarudi Tanzania terehe hiyo ambayo itakuwa ni Jumamosi wiki hii, hata hivyo Lissu sasa anasema bado anasubiri kupata ridhaa ya madaktari wake iwapo anaweza kurudi nyumbani.
'Nilishasema kwamba ninasubiri nipate uamuzi wa mwisho wa madaktari wangu, nasubiri waniambie sasa unaweza kwenda nyumbani. Wakiniambia hivyo nitaanza kupanga mipango ya safari ya nyumbani.
'Sio bayana maana daktari wangu hajaniambia bado kwamba sasa nenda nyumbani, hajaniambia bado.' Lissu ameiambia BBC Swahili katika mahojiano.
Mnamo mwezi Mei mwaka huu wakati akizungumza kwa njia ya simu na kupitia runinga ya Chadema mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe katika makao makuu ya Chadema, Lisu amesema kuwa atarudi nchini Tanzania siku hiyo ili kuadhimisha kushambuliwa kwake.
''Nitatua tarehe saba mwezi septemba 2019 kwenye ardhi ya tanzania kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa nitakuwepo, alisema Tundu Lissu
Tangazo hilo liliwafurahisha sana wanachama wa chama hicho waliokuwa katika makao makuu ya chama hicho.
Miraji Mtaturu aapishwa rasmi kuwa mbunge wa Singida Mashariki
Katika hatua nyingine Mwanasiasa huyo wa upinzani ambaye pia alikuwa anashikilia kiti cha ubunge wa Singida Mashariki, amesema atapinga uamuzi wa kuapishwa hii leo kwa Miraji Mtaturu, kutoka Chama Cha Mapinduzi, CCM, kama mbunge mpya wa eneo hilo.
Mtaturu amechukua kiti hicho cha ubunge ambacho kilishikiliwa na Tundu Lissu mpaka alipovuliwa wadhifa huo na Spika wa bunge Job Ndugai mnamo Juni 28 mwaka huu.
Lissu amesema: ''Huo mgogoro wa mimi kuvulia kiti cha ubunge bado ni mbichi kabisa ...ugomvi wetu ni uamuzi wa Spika alifanya sahihi au alikosea, mahakama ikisema spika alikosea Miraji Mtaturu sio mbunge''.
Amesema yaliyotokea leo asubuhi hayakumshangaza wala hayamhangaishi kwa kitu chochote ''Spika ametangaza tangu Januari mwaka huu kwamba atanifuta ubunge kwa hiyo ilivyotekea mwezi wa Juni kwamba atanifuta wala hainishangazi hata kidogo'', amesema Bwana Lissu.
Mwanasheria huyo na mwanasiasa wa upinzani ameongeza kuwa ''Sheria zetu ziko wazi mwenye kauli ya mwisho katika masuala ya migogoro ya kisheria ni mahakama ya rufaani ya Tanzania, tusubiri mahakama kuu itaamua nini Jumatatu halafu tutaamua kama kwenda mahakama ya rufaa au tunaridhika na uamuzi wa mwaka huu''.
Alipoulizwa juu ya ikiwa bado ana nia ya kugombea urais amesema, iwapo chama chake pamoja na vyama rafiki vitampa wito wa kuviwakilisha katika kinyanganyiro cha urais mwakani, atagombea na kuongeza kuwa bado hajabadilisha msimamo wake hata kidogo.
''Katiba ya Tanzania inasema uwe umepatikana na hatia ya kosa kwa mujibu wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma. Hatia ni kwamba umeshtakiwa, ukajitetea, utetezi wako haukutosha ukapatikana na makosa ndio katiba ya Tanzania itakuwa inakuzuwia'' alifafanua Bwana Lissu.
Alipoulizwa ikiwa kwa miaka 2 baada ya kushambuliwa hadhani kwamba wakazi wa Singida mashariki wana haki ya kupata mbunge mwingine alisema:
''Mimi sikuugua malaria nilipigwa risasi katikati ya vipindi vya bunge nikiwa bungeni.''
Spika wa bunge la Tanzania Job Ndungai alimvua kiti cha ubunge Tundu Lissu
Image captionSpika wa bunge la Tanzania Job Ndungai alimvua kiti cha ubunge Tundu Lissu
Tundu Lissu amekuwa nchini Ubelgiji akipokea matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana mchana wa Septemba 7 mwaka 2017.
Lakini wakati akiwa huko Spika Ndugai alimvua ubunge kwa madai kwamba hakuwa ametoa taarifa rasmi ya alipo, na pia hakuwa amejaza fomu za mali na madeni ya viongozi wa umma.
Mtaturu alitangazwa mbunge mteule wa jimbo hilo kwa kupita bila ya kupingwa katika hatua za awali za matayarisho ya uchaguzi mdogo baada ya wagombea 12 wa vyama vya upinzani kutorejesha fomu.
Uchaguzi huo mdogo ulikuwa ufanyike Julai 31, lakini haukufanyika tena kutokana na wapinzani kutokurejesha fomu zao.
Hata hivyo, kuna kesi mahakamani ambayo inaweza kuathiri kiapo cha Mtaturu hii leo, pale ambapo maamuzi yake yatakapotolewa wiki ijayo.
Kesi hiyo imepelekwa mahakamani na Lissu akipinga kuvuliwa ubunge wake.

Yalijoriri mahakamani jana

Hapo jana mawakili wa Lissu walitarajia kuzuia kuapishwa kwa Mtaturu hii leo hadi pale kesi hiyo itakaposikizwa na kuamuliwa.
Hata hivyo, Jaji Sirillius Matupa wa Mahakama Kuu ya Tanzania alilikataa ombi hilo la mawakili wa Lissu akisema katika kesi za ubunge hata kama mtu ameapishwa anaweza kuvuliwa ubunge pamoja na kiapo chake.
Kesi hiyo hapo jana iliunguuma mpaka saa tatu kasoro robo usiku ambapo Jaji alitangaza maamuzi yake juu ya ombi la kiapo cha Mtaturu.
Jaji Matupa amesema kuhusu maombi rasmi ya Lissu kupinga kuondolewa katika ubunge yatatolewa Septemba 9, 2019.
Lissu amefungua maombi chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Alute Mughwai, ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo, akitaka kurudishiwa ubunge wake.
Lissu anapinga vikali kuvuliwa wadhifa wake akidai kuwa amefutwa ubunge huku ikifahamika wazi kuwa amekuwa nje kwa matibabu tangu tarehe 7 mwezi Septemba mwaka 2017, baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana.
Mwanasiasa huyo hapo awali aliiambia BBC kuwa alitarajia hatua zilizochukuliwa na Spika dhidi yake kwa sababu alishasema kwa hiyo ilipotokea mwezi wa sita wala haikuwa ajabu.
''Mtu ambaye alishakuwa na nia ya kunifuta ubunge nisingeweza kumzuia, vinginevyo labda ningesema niachane na habari ya matibabu nirudi Tanzania''.

Post a Comment

0 Comments