Viongozi wanaotoa ahadi hewa, waandaliwa mkakati


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Damas Ndumbaro amesema serikali imekuwa ikifanya vikao vya majadiliano kuhusu viongozi mbalimbali wanaokuja nchini  kutoka nje na kutoa ahadi bila kuzitekeleza ili kufikia muafaka.

Dk. Ndumbaro ameyasema hayo, bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Tauhida Cassian, maelezo ya serikali juu ya viongozi hao wanaokuja nchini.

“Je, serikali ina maelezo gani juu ya viongozi wanaokuja Tanzania na kutembelea baadhi ya maeneo na kisha wanapokuta miradi ya wananchi huahidi kusaidia na baadaye kushindwa kutimiza ahadi zao,” amehoji mbunge.

Akijibu swali hilo, Dk. Ndumbaro amesema ahadi ambazo hutolewa na baadaye kushindwa kutimizwa wizara huratibu vikao vya majadiliano vinavyoshirikisha wahusika pamoja na wizara za kisekta na taasisi za kiserikali ili kupata muafaka juu ya suala husika.

“Tanzania imekuwa ikipokea viongozi wageni kutoa nje ya nchi katika makundi mawili, yaani viongozi hao hutembelea kwa safari za kiserikali na binafsi ambapo hupata fursa ya kuona miradi ya wananchi.

“Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikaino wa Afrika Mashariki, ina jukumu la kuratibu na kusimamia safari za kikazi kutoka mataifa ya kigeni ikiwa ni pamoja na kufuatilia utekelezaji wa ahadi mbalimbali zinazotolewa na viongozi hao kwa kushirikiana na wizara za kisekta na taasisi kiserikali,” amesema.

Post a Comment

0 Comments