tangazo

Samatta akumbana na panga kali kwenye mshahara wake, akatwa asilimia 25

HUKU akiendelea kujifungia ndani kukwepa maambukizo ya virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu (COVID-19) kama ilivyo kwa wachezaji wenzake, mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, amekumbana na panga kali kwenye mshahara wake

Hata hivyo, panga hilo halitatembezwa kwenye mshahara wa Samatta pekee, bali kwa wachezaji wote wa Aston Villa, na benchi la ufundi la kikosi cha kwanza na viongozi wakuu wa klabu hiyo wote wamekubali kukatwa kiasi hicho katika mishahara yao kila wiki kutokana na janga la COVID-19 ili kuisaidia klabu hiyo kusonga mbele, taarifa ya Aston Villa ilieleza juzi, Jumamosi.

Villa inakuwa klabu ya hivi karibuni kutoka Ligi Kuu England kutangaza uamuzi huo wa wachezaji, baada ya Southampton, West Ham United, Watford na Sheffield United kuchukua hatua kama hiyo.

Shughuli zote za soka England zilisimama kuanzia mwezi uliopita kutokana na mlipuko wa janga la virusi vya corona.

"Wachezaji wa kikosi cha kwanza, makocha wa kikosi cha kwanza na viongozi wakuu wote wamekubali kupunguzwa kwa mishahara yao kwa asilimia 25 kwa kipindi cha miezi minne kuisaidia klabu katika kipindi hiki cha kutokuwa na uhakika," Ofisa Mtendaji Mkuu wa Villa, Christian Purslow alisema.

Aliongeza kuwa, mapitio zaidi yatafanyika mwishoni mwa kipindi cha miezi minne.

Arsenal ilitangaza makato ya asilimia 12.5 kwa wachezaji wake na viongozi wa benchi la ufundi tangu ligi hiyo iliposimama, wakati Liverpool, Tottenham Hotspur na Bournemouth walibadilisha uamuzi wao wa awali ili kuwachanganya wafanyakazi wasiokuwa wachezaji kutokana na kukosolewa.

Mapema Jumamosi, Norwich City ilitetea uamuzi wake kwa wafanyakazi, wakati Chelsea ilisema wachezaji wao wa kikosi cha kwanza hawatakumbana na panga hilo la mishahara.

Post a Comment

0 Comments