Zimbabwe yaadhimisha miaka 40 ya uhuru

Imetimia miaka 40 leo (18.04.2020) tangu bendera ya Uingereza iliposhushwa nchini Zimbabwe, na ya taifa jipya huru ikapandishwa kuashiria uhuru wa nchi hiyo, miongoni mwa chache zilizokuwa zikibakia chini ya ukoloni.

    
Zimbabwe | Emmerson Mnangagwa | Eternal Flame of Freedom (Getty Images/AFP/J. Njikizana)
Miongo minne tangu siku hiyo ya uhuru, Wazimbabwe wengi wanasema hakuna cha kusherehekea, kufuatia miaka mingi ya utawala wa kikandamizaji wa Rais Robert Mugabe.
Kawaida maelfu ya raia wa Zimbabwe hushiriki katika hafla za kuadhimisha sikukuu ya uhuru kila tarehe 18 Aprili, kuwaenzi mashujaa waliojitolea kupigania uhuru huo ambao hatimaye ulipatikana mwaka 1980. Kila mwaka wakati wa maadhimisho hayo, ''mwenge wa uhuru wa daima'' huashwa kama ishara ya matumaini ya mustakabali mwema kwa taifa.
Ingawa mwaka huu sherehe hizo zimeahirishwa kutokana na kitisho cha virusi vya corona, hata raia wengi walikuwa hawana hamu ya kushiriki.
Kutoka matumaini hadi kukata tamaa
Wazimbabwe wengi walikuwa na matumaini makubwa pale nchi yao ilipotangaza uhuru wake kutoka ukoloni wa Waingereza ulioanza mwaka 1890 na kudumu hadi 1979, wakati huo ikiitwa Rhodesia.
Miaka ya mwanzo ya uhuru ilikuwa yenye neema; uchumi uliimarika, kulikuwepo uvumilivu wa kisiasa, nchi ilikuwa na demokrasia shirikishi, na amani, haki na maridhiano vilishuhudiwa.
Umstrittene Wahlen haben die simbabwische Politik behindert (DW/P. Musvanhiri)
Kaburi la askari asiyejulikana kwenye makumbusho ya mashujaa mjini Harare, Zimbabwe
Utawala wa Robert Mugabe, Waziri Mkuu wa kwanza wa nchi hiyo na shujaa wa ukombozi, alijenga mfumo bora wa elimu na afya ambavyo vilikuwa mfano kwa bara zima, wakati huo Zimbabwe ikichukuliwa kama ghala la chakula kwa Afrika. Lakini yote yalibadilika baada ya Mugabe kung'ang'ania madarakani kwa muda mrefu.
Hivi sasa uchumi wa Zimbabwe umesambaratika, na raia wake wanapata taabu hata kupata mahitaji ya msingi kama chakula, licha ya kwamba taifa lao lina utajiri mwingi wa asili, kama dhahabu, almasi na chuma ghafi.
Tabaka la viongozi wasio na dhamira safi
Mchambuzi mmoja wa masuala ya kisiasa nchini humo Alexander Rusero ameiambia DW kuwa ''serikali haionyeshi dhamira yoyote ya kurekebisha makosa yaliyofanyika'', na kuongeza kuwa huwezi kuzungumzia uhuru ambao sio zaidi ya wimbo wa taifa na bendera tu.
''Hakuna fursa sawa kwa wote katika matumizi ya raslimli za nchi. Kwa mtu ambaye kila aamkapo hana uhakika wa maji safi, chakula na nishati ya umeme, uhuru hauna maana yoyote.'' Amesema Rusero.
Simbabwe | Verteilung von Hilfsgütern des Welternährungsprogramms der UN in Mudzi (picture-alliance/AP Photo/T. Mukwazhi)
Wazimbabwe wengi hivi sasa wanategemea msaada wa chakula kutoka kwa wahisani
Lakini kwa chama cha ZANU-PF ambacho kimeitawala Zimbabwe tangu uhuru, ukombozi kutoka utawala wa Wazungu wachache ni sababu tosha ya kusherehekea. Mkurugenzi wa habari wa chama hicho Tafadzwa Mugwadi ameiambia DW katika mahojiano kuwa ingawa ni kweli kuwa yamekuwepo matatizo ya ndani, maadhimisho ya miaka 40 ya uhuru ni kielelezo cha ushindi.
''Kuna mgogoro baina ya vizazi, kati ya wazee wanaohisi kuwa na nafasi zaidi kutokana na ushujaa wao katika ukombozi wa nchi, na kizazi kipya ambacho matarajio yake yamekatishwa tamaa.'' alisema mchambuzi Alexander Rusero.
Ndoto iliyogeuka jinamizi
Watu waliozaliwa baada ya uhuru wanaamini kwamba maendeleo ya Zimbabwe yamevurugwa na kizazi kilichotangulia ambacho kimeng 'ang'ania madarakani mtindo sawia na watawala wa kikoloni.
Rais wa sasa Emmerson Mnangagwa,alieingia madarakani baada ya kuangushwa kwa Robert Mugabe mwaka 2018, ni miongoni mwa waliopigana vita vya ukombozi wa Zimbabwe. Wenzake wengi walioshiriki katika vita hivyo bado wanashikilia nyadhifa muhimu ndani ya jeshi, polisi, na kwenye taasisi muhimu za serikali na ndani ya chama tawala.
Kiongozi wa upinzani, Nelson Chamisa, ambaye pia ni kijana, aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter kwamba miaka ya 40 ya uhuru inawakilisha ndoto iliyovunjika.

Post a Comment

0 Comments