Trump: Athari za COVID-19 ni zaidi ya mkasa wa Septemba 11

Kwa mara nyingine rais wa Marekani Donald Trump ameishambulia China kwa jinsi ilivyoshughulikia mlipuko wa virusi vya corona huku akisema janga hilo limekuwa na madhara makubwa kwa Marekani.

  
Rais Trump amewaambia waandishi habari mjini Washington kuwa ugonjwa wa COVID-19 umeiathrii Marekani  kwa kiwango kikubwa kuliko mashambulizi ya mabomu dhidi ya kambi ya kijeshi ya Pearl Harbor ya mwaka 1941 au tukio la kigaidi la Septemba 11.

Hayo ni moja ya matukio makubwa kabisa na yaliyosababisha athari pana katika historia ya Marekani.

Mashambulizi ya Japan kwenye kambi ya Pearl Harbor iliyokuwepo Hawaii  yaliilazimisha Marekani kuingia katika vita kuu ya pili ya dunia huku mkasa wa Septemba 11 uliwauwa wamarekani zaidi ya 3,000 na kuisukuma Washington kuanzisha operesheni dhidi ya ugaidi nchini Iraq, Afghanistan na kwingineno.

Trump ameilaumu China akisema virusi vya corona visingesababisha athari kubwa iwapo Beijing ingefanikiwa kuvidhibiti kikamilifu vilipozuka mwishoni mwa mwaka uliopita.

Huo ni mfululizo wa lawama za Marekani kwa China kuhusu virusi vya corona na katika siku za karibuni rais Trump na viongozi wake waandamizi wamesema wana ushahidi kuwa virusi vya corona vilizuka kutoka maabara moja mjini Wuhan nchini China.

Madai hayo yamepingwa vikali na China na wanasayansi bado wanaamini virusi hivyo vialinzia kwa wanyama kabla ya kuingia kwa binadamu hususan kupitia soko la nyamapori la mjini Wuhan.

Hadi sasa zaidi ya watu 73,000 wamekufa nchini Marekani kutokana na ugonjwa wa COVID-19 na mkuu wa zamani wa taasisi ya kuzuia magonjwa nchini humo amebashiri idadi ya vifo inaweza kufikia 100,000 mwishoni mwa mwezi Mei.

Tom Frieden ametaka wabunge kujitayarisha kwa vita ngumu na ya muda mrefu ya kuudhibiti ugonjwa wa COVID-19 ma ametoa wito wa kuongeza uwezo wa kufanya vipimo.

Hadi sasa virusi vya corona vimesababisha vifo vya watu 260,000 kote duniani huku wengine karibu milioni 3.7 wameambukizwa maradhi ya COVID-19.

Nchini Uingereza waziri mkuu Boris Johnson amesema wiki inayokuja anaweza kuanza kulegeza viuzuzi vilivyowekwa nchini nzima kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

Akizungumza kwa mara kwanza Bungeni tangu alipotoka hospitali alikolazwa baada ya kuambukizwa virusi vya coorna, Johnson amesema serikali yake itapitia takwimu zilizopo kabla ya kutangaza hatua inayofuata siku ya Jumapili.

Johson ametoa matamshi hayo siku moja baada ya Uingereza kuizidi Italia na kuwa ya kwanza barani Ulaya kwa idadi kubwa ya vifo vilivyotokana na virusi vya corona ambavyo vimefikia watu 32,000.

Katika hatua nyingine wakati Ujerumani imetangaza jana mipango ya kurejea kwa hali ya maisha ya kawaida - ikiwemo kuruhusu tena ligi ya kandanda kuanza kutimua vumbi Mei 15 - Umoja wa Ulaya umebashiri kutashuhudiwa mdodoro mbaya wa uchumi kutokana na athari za virusi vya corona.

Post a Comment

0 Comments