tangazo

Angela Nzilani aligundua alikua na mke mwenza aliyeishi na mumewe miaka 10

Maisha aliyoyapitia Angela Nzilani yamemfanya awe mtoa ushauri nasaha kwa watu ambao wako kwenye mahusiano ya kimapenzi.
Alikua na umri wa chini kidogo ya miaka 20 alipokutana na mwanaume ambaye anasema alimpenda sana kiasi kwamba, alihisi kuwa huyo ndiye angelikua mumewe wa kuishi nae maisha yake yote hapa duniani.
Angela Nzilani ni mwanamke kutoka Kenya ...kama mwanamke mwingine yoyote yule, alijipata katika dimbwi la mapenzi na mwanaume aliyempenda. ''Tulikutana wakati nilipokua nikisoma chuo kikuu, alinizuzua kimapenzi kweli kweli'', anasimulia Angela katika mazungumzo na BBC.
Bi Angela Nzilani ni mama wa watoto wawili wa kiume, matukio ya maisha yake yamembadilisha yeye na akaanza kuwa mtoa ushauri nasaha kwa watu ambao wako kwenye mahusiano ya kimapenzi.
Alipokuwa na umri wa miaka ya chini kidogo kama ishirini tayari alikuwa amepata mtoto na alipokuwa chuo kikuu alikutana na mwanamume mmoja ambaye walipendana na kuanza safari ya mapenzi.
Lakini Angela anasema : ''Nilikua mwanamke wa kupenda raha na sikua nafanya maamuzi ya busara...na kutokana na hilo nilipopata ujauzito, mwanaume hakuwa tayari kufunga ndoa na mimi na hapo ndipo uhusiano wetu ulikwisha...Ninakiri kuwa nilikuwa mwanamke wa kurukaruka huku na kule na si kuwa nimepanga maisha yangu vizuri, kwa hiyo sio ajabu kuwa uhusiano wangu wa kwanza ulifeli ",Angela anakiri.
Angela alijaliwa kujifungua vema mtoto wake wa kwanza wa kiume kutokana na uhusiano huu na akaendelea na maisha yake na mwanae.
Maisha yake Angela yaliendelea vizuri kwani aliingia kwenye biashara ya ujenzi na alikuwa na kandarasi mbali mbali, alijaliwa fedha kiasi cha haja: ''Sikua na shida ya fedha, nilikua na gari na nilikua ninaishi katika nyumba nzuri tu''

Mahaba na mwanaume wa pili.

Licha ya kuwa na maisha mazuri Angela alihisi kuwa kuna kitu anachokikosa maishani mwake...mpenzi wa kumdekeza maishani na baba wa mtoto wake.
Waswahili husema majuto ni mjukuu... Angela alianza kupanga maisha yake upya na alimua kuwa atatafuta mpenzi mwingine lakini mara hii kwa misingi ya ndoa.
Kwa kuwa Angela alitamani sana kuwa na mpenzi aliamua kuishi na marafiki wa mumewe nyumbani kwakeHaki miliki ya pichaANGELA NZILANI
Image captionKwa kuwa Angela alitamani sana kuwa na mpenzi aliamua kuishi na marafiki wa mumewe nyumbani kwake
Haikuchukua muda mrefu, Angela alikutana na mwanaume kutoka nchi moja ya magharibi mwa Afrika ambaye anasema kuwa alimuonyesha mahaba na maneno na kwa vitendo: ''Penzi lake lilinipumbaza na nikashawishika kuwa huyo ndie alikua mwanaume niliyekua ninamtafuta'', anasema.
Mapenzi yao yalinoga na baada ya mwezi mmoja tu mpenzi wake alikuwa amehamia katika nyumba ya Angela na mwanae.
Angela anasema kuwa mpenzi wake alikuwa nchini kenya kama kocha wa mpira wa miguu na alikuwa anahusika sana na kuzitafutia wachezaji wa soka kutoka Magharibi mwa Afrika timu za soka na msimu waliokutana ulikuwa sio mzuri sana kifedha kwa mpenzi wake.
Kwa kuwa Angela alitamani sana kuwa katika mahusiano ya ndoa aliona ni kheri yule mpenzi wake pamoja na wanaume wengine watano waliokuwa wanaishi na mpenzi wake wahamie nyumba yake kwa kuwa ilikuwa kubwa. Huo ukawa mwanzo wa safari ya maisha yake ya ndoa...
''Mimi nilikuwa nafanya kila kitu kwa nyumba, fedha zangu zilitumika katika kulipa kodi, kununua chakula na kugharamia mahitaji ya mpenzi wake na wale wanaume wengine watano waliokuwa wanaishi na sisi'' Angela anakumbuka.
Baada ya mwezi mmoja Angela alipata ujauzito na anasema kuwa mpenzi wake alifurahi sana, lakini baada ya miezi miwili mimba ile ilijiavya tumboni. Haikuwa rahisi kwake na kwa mpenzi wake ambaye sasa alimtambua kama mume wake kukubali hayo kwa hio baada ya mwezi mwengine mmoja hivi angela alishika mimba nyengine.
Wakati huo biashara ya ujenzi yaAngela ilikuwa imeanza kuporomoka kwa kasi kwani mapato yalikuwa yameshuka mno. Kipindi hicho pia Angela anasema kuwa mumewe alianza kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanawake wengine hapa na pale ambao aliwatumia kupata fedha.
''Sio mara moja wala mbili nimepokea simu za wapenzi wa mume wangu wakinitusi na kunikemea, wakitaka wajulikane kuwa walikuwa wapenzi wa mume wangu'' Angela alisema.
Angela anasema kuwa mume wake alikuwa anampenda mwanae wa kiume japo hakuwa wake kibaiolojiaHaki miliki ya pichaANGELA
Image captionAngela anasema kuwa mume wake alikuwa anampenda mwanae wa kiume japo hakuwa wake kibaiolojia
Kwa kuwa alikuwa na mimba aliona avumilie na pia kwa kuwa alikuwa ameamua kuwa kwa mabaya na mazuri atakaa kwenye ndoa ile.
Angela anasema kuwa mume wake alimpenda mwanae wa kiume japo hakuwa wake kibiolojia: Niliona afadhali nivumilie angalau wanangu wapate baba yao na mimi nipate mume''.
Kwakua mapato yake yalishuka sana na ikawabidi wahame kutoka nyumba ya kifahari waliyokuwa wanaishi, pamoja na wale wanaume watano ambao walikuwa jamaa wa mumewe, hali haikuwa rahisi, wakati huo kwani Angela alikuwa anakaribia kujifungua.
Hapo ndipo mumewe alimshauri kuwa arejee nchini kwao Ghana kutafuta riziki, na baada ya muda Angela na wanae watasafiri huko, ilimbidi auze gari lake na pia kutumia fedha alizokuwa ameweka akiba, ilikufanikisha safari ya mumewe nchini mwao.
Miezi mitatu baada ya mumewe kurudi Ghana Angela alijifungua mtoto wa kiume na ikawa vigumu kwake kupata fedha za kulipia garama za hospitali, ilibidi awafukuze wanaume marafiki za mumewe kwa kuwa maisha yalianza kuwa magumu sana.
''Mume wangu aliahidi kuwa angetuma fedha zetu kusafiri hadi nchini mwao huko Ghana, kwa hiyo tulianza mipango hiyo na ilinilazimu nianze kuuza kila kitu nilichokuwa nacho ''Angela anakumbuka.
Pia alihama kutoka nyumba aliyokuwa anapangisha na akahamia kwa dada yake kwani alikuwa amesalia na wiki mbili tu kusafiri kuungana na muemewe, kulingana na walivyokua wamepanga na mume wake.
Angela alihisi mapenzi yalikua kama mchezo wa kuigizaHaki miliki ya pichaANGELA NZILANI
Image captionAngela alihisi mapenzi yalikua kama mchezo wa kuigiza

Mipango ilivyoharibika

Siku ya kusafiri ilipowadia mume wake hakuwa na fedha za kuwatumia yeye na wanae wa kiume kwa ajili ya safari ya kwenda Ghana. Ilikuwa wakati mgumu sana kwake.
Kana kwamba haitoshi wakati akifikiria juu ya jambo la kufanya alipokea simu moja ambayo anasema hatawahi kuisahau: "Nilipokea simu kutoka nchini ya Ghana, na sauti ya mwanamke ikanieleza kuwa huyo mume wako amekuwa akikudanganya hana mke, lakini nimekuwa mke wake kwa muda wa miaka 10 "Angela alisema.
Hakua na nguvu hata za kuzungumza alipomuomba yule mwanamke amtumie ushahidi wa anayosema kuwa kama kweli alikuwa mumewe kwa miaka kumi, yule mwanamke alimtumia picha za harusi kwa simu, na ilikuwa bayana alikuwa amedanganywa na kweli ni mume wa mtu.
''Nilipompigia simu na kumuuliza kuhusu madai ya mwanamke yule, alikana kidogo kisha akakubali kuwa yule alikuwa mkewe, alikuwa hana maneno ya kusema ila kulia lia akiomba nimsamehe'', anakumbuka Angela.
Hadi hapo Angela alihisi kana kwamba hawezi kuendelea na uhusiano huo tena.
Angela anasema kuwa ni rahisi mno kwa mwanamke ambaye anatamani kupendwa kuhadaiwa na wanaume.Haki miliki ya pichaANGELA NZILANI
Image captionAngela anasema kuwa ni rahisi mno kwa mwanamke ambaye anatamani kupendwa kuhadaiwa na wanaume.
Kila anapokumbuka kuwa alikuwa ameuza kila kitu akisubiri kusafiri kuungana na mtu aliyeamini kuwa mumewe, huhisi kana kwamba alikuwa kwenye mchezo wa kuigiza.
Alijiahidi kuwa uhusiano huo lazima ufikie ukomo kwa kuwa katika mipangilio ya maisha yake, Angela alikuwa hataki kuwa mke wa pili yaani kuharibu uhusiano wa mwanamke mwenzake .
Imekuwa ni safari kwa Angela japo anakiri kumsamehe baba ya mtoto wake kwa yote aliomhadaa na anasema kuwa ni rahisi mno kwa mwanamke ambaye anatamani kupendwa kuhadaiwa na wanaume mwenye wapenzi wengi, au wanaume wanaotafuta mali kutoka kwa wanawake wenye kiu ya mapenzi .
Kwa sasa Angela yuko kwenye shirika linalosaidia watu kujitambua, kujielewa na kufahamu mwelekeo wao wa maisha, lakini haya yote aliyagundua baada ya kupitia changamoto nyingi za mahaba na aliyekuwa mume wake.

Post a Comment

0 Comments