tangazo

Askofu Nyanza wa TMC Manyara akabidhi vifaa kinga vya Corona

Tanzania Methodist Church(TMC) jimbo la Manyara Samweli Nyanza amekabidhi msaada wa vifaa vya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona kwa taasisi za umma na makanisa vyenye thamani ya shilingi Milioni 12.84.

Alikabidhi msaada huo  kwa mkuu wa wilaya ya Babati Elizabeth Kitundu katika makao makuu ya Dayosisi ya Manyara, Kiongozi huyo wa kiroho alisema Kanisa la TMC limeamua kuvunja bajeti zote za kanisa lao ili kutoa vifaa hivyo ili kupambana na corona.

Alivitaja vifaa walivyokabidhi ni pamoja na vitakasa mikono, barakoa, ndoo za kunawia, sabuni, beseni ndogo za kunawia na kutoa vyerehani viwili kwa wanawake wa kanisa hilo ili wavitumie kushona barakoa za kutosha kusaidia jamii.

Taasisi zilizopewa vifaa hivyo ni ofisi ya mkuu wa wilaya, ofisi ya mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Babati, ofisi za mitaa, Hospitali ya Mji wa Babati Mrara, Kituo cha wazee Magugu,Kituo cha redio cha Smile Fm na makanisa marafiki na makanisa ya TMC.

Nyanza alisema ameamua kutoa msaada huo baada ya kuona kuna shida kidogo makanisani licha ya askofu mkuu wa kanisa hilo Yusuph Bundala kutoa waraka wakuwataka ibada ziwe fupi au ziongezwe ili kuepuka misongamano.

Alitumia fursa hiyo kupiga marufuku mashemasi kukaa viti vya mbele wakati wao ndio wana jukumu la kuwalinda waumini huku akitangaza kuwafuta kazi watakakiuka masharti.

Askofu huyo alisema kutokana na ugonjwa huu akifika nyumbani kwake anavulia nje nguo ili asiingize ndani maambukizi huku akidai mke wake hatoki ndani ili asipate maambukizi.

Naye ofisa afya wa Mji wa Babati Aretas Laurent akizungumza na waumini hao aliendelea kutoa tahadhali na kusema kua ugonjwa huu unaambukiza sana kupitia macho, pua na macho na dalili kuu ni joto kupanda.

Mtaalamu huyo aliitaka jamii kuacha kuona kila ugonjwa ni corona au kila anayekufa.

Mkuu wa wilaya ya Babati Elizabeth Kitundu baada ya kupokea msaada huo alilishukru kanisa hilo na akasema bado kuna tatizo kwenye masoko na minada kama hamna ulazima waache kwenda.

Kitundu aliwataka wananchi kuacha kusikiliza taarifa zenye upotoshaji ambazo hazina uhakika  badala yake wawafatilie wasemaji wakuu wa serikali.

Post a Comment

0 Comments