tangazo

Barcelona Waanza Mazoezi

MABINGWA wa La Liga Barcelona jana Ijumaa wakiwemo Lionel Messi, Luis Suarez na wachezaji wengine wa Barça, walirejea kwenye Uwanja wao wa mazoezi uliopo katika mji mkuu wa Catalan.

Barca walikuwa wakiendesha mazoezi kwa wachezaji binafsi, huku kikosi kikigawanywa katika sehemu tatu uwanjani wakitekeleza agizo la kutokaribiana baada ya kikosi kupimwa na kufanyiwa taratibu zote za afya. Wachezaji waliambiwa kuwasili moja kwa moja uwanjani wakiwa na vifaa vyao vya mazoezi, na kurudi mara moja nyumbani baada ya kumaliza mazoezi yao bila ya kuingia katika vyumba vya kubadilishia nguo.

Walifanya mazoezi kwa muda tofauti na wataendelea kufanya hivyo leo Jumamosi. Mabingwa hao wa La Liga walitweet picha zao wakifanya mazoezi kwa mara ya kwanza tangu kusimamishwa kwa shughuli zote za michezo kutokana na virusi vya corona.

Mshambuliaji Suarez, ambaye alikuwa nje ya uwanja tangu Januari kutokana na maumivu ya goti, alitweet: “Ni vizuri kurudi!” Hispania ni moja ya nchi za Ulaya zilizoathirika sana na maambukizi na Covid-19, ingawa La Liga wana matumaini mashindano ya ushindano kurejea katikati ya Juni. Wakati huohuo, Wachezaji watano wa La Liga na Ligi Daraja la Pili, wamekutwa na virusi vya corona, imeelezwa.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Catalan, wachezaji watatu wa Ligi Kuu na wawili wa Daraja la Pili wamekutwa na virusi hivyo. Wachezaji hao walikutwa na virusi hivyo katika vipimo vya kwanza wakati Ligi Kuu ya Hispania, La Liga ikielekea kurudi. Majina ya wachezaji hayo hayakutajwa, ambapo inaelezwa kuwa inatarajia wachezaji zaidi kukutwa na virusi hivyo wakati vipimo vitakapoendelea kufanywa, imetangazwa. Wakati hata klabu za wachezaji hao hazikutajwa, lakini RAC1 imethibitisha kuwa hakuna mchezaji yoyote kutoka Barcelona aliyekutwa na virusi hivyo.

Vipimo vya Covid-19 vinafanywa kwa kila mchezaji anayecheza La Liga, pamoja na benchi la ufundi na wafanyazi wote ambao wanagusana na wachezaji. Wakati huohuo, kocha wa Leganes Javier Aguirre alibainisha kuwa La Liga wamepanga kuendelea Juni 20 na kumalizika Julai 26.

Post a Comment

0 Comments