Corona yaporomosha mapato ya utalii

Kutokana na virusi vya corona vinavyoendelea kuisumbua dunia, Wizara ya Utalii na Maliasili imesema mapato katika sekta hiyo yameshuka kutoka Sh trilioni 2.6 zilizotarajiwa kukusanywa hadi kufikia Sh milioni 598.

Pia taasisi zilizokadiriwa kukusanya zaidi ya Sh bilioni 132.1 zinatarajia kukusanya Sh bilioni 33.5 ikiwa ni anguko la asilimia 75.

Vilevile, Serikali imesema kama hali haitatulia hadi Oktoba, ajira za moja kwa moja katika sekta ya utalii zitashuka kutoka 623,000 hadi kufikia 146,000 na watalii watashuka kutoka 1,867,000 waliotarajiwa hadi 437,000.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2020/21.

Dk. Kigwangalla alisema sekta ya utalii imeathirika kwa kiwango kikubwa kutokana na corona.

“Moja ya sekta muhimu zilizoathiriwa ni utalii. Sekta hiI kabla ya madhara hayo ilikuwa inachangia asilimia 25 katika mapato yote ya kigeni inayopata nchi yetu.

“Sekta hii imeathiriwa zaidi kutokana na ukweli kwamba inategemea zaidi mapato ya watalii wanaotoka nje ya nchi, ambao kwa sasa kutokana na ugonjwa huu, wameshindwa kusafiri na wengi wao wamesitisha safari za kuja nchini kutalii,” alisema Dk. Kigwangalla.

Alisema wizara ilifanya tathmini ya awali (rapid assessment) iliyojikita katika kipindi cha tangu ugonjwa huo uanze hadi Aprili 6, mwaka huu.

Dk. Kigwangalla alisema tathmini hiyo ilibaini kuwa madhara makubwa ya corona katika sekta ya utalii yalianza kuonekana mwanzoni mwa Machi, tofauti na Februari na Januari, mwaka huu ambapo hali ilikuwa shwari. Alisema tathmini ilibaini mashirika 13 ya ndege yalisitisha safari za kuja nchini tangu Machi 25, mwaka huu hivyo kuondoa uwezekano wa kuendelea kupata watalii kutoka nje ya nchi.

Dk. Kigwangalla alisema mashirika yaliyositisha safari zake ni pamoja ni Emirates, Swiss, Oman Air, Turkish, Egyptian Air, South African Airways, Rwandair, Qatar, Kenya Airways, Uganda Airlines, Fly Dubai na KLM.

“Vilevile, kampuni yetu ya ndege ya Air Tanzania imesitisha safari za nje ya nchi.

“Madhara haya yanaonekana kuwa makubwa zaidi ambapo tayari kuna dalili za kushuka kwa mapato yaliyotarajiwa kukusanywa na taasisi kubwa zilizo chini ya wizara ambazo ni Tanapa (Mamlaka ya Hifadhi za Taifa), NCAA (Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro), TFS (Wakala wa Huduma za Misitu) na Tawa (Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania).

“Kwa mfano, katika mwaka 2020/2021 Tanapa ililenga kukusanya Sh bilioni 363.9, lakini kutokana na hali inavyoendelea, makisio sasa yanakadiriwa kuwa Sh bilioni 64 au chini ya hapo,” alisema Dk. Kigwangalla.

Alisema NCAA ilikadiria kukusanya Sh bilioni 162.7, kwa sasa itakusanya Sh bilioni 58, TFS ilikadiria Sh bilioni 153.6, sasa ni Sh bilioni 121 na Tawa ilikadiria Sh bilioni 58.1 sasa ni Sh bilioni 22.

“Upungufu huo wa mapato ni mkubwa kwa sekta, na unaweza kusababisha baadhi ya taasisi za uhifadhi zilizo chini ya wizara kushindwa kujiendesha ikiwa ni pamoja na kulipa mishahara.

“Katika kukabiliana na hali hiyo, wizara imeendelea kuwashirikisha wadau wa sekta ili kuweka mikakati ya namna ya kuisaidia sekta isiathirike zaidi,” alisema Dk. Kigwangalla.

Post a Comment

0 Comments