tangazo

CWT mambo ni moto, mwalimu atangaza nia ya kumng'oa Rais wake

Wakati Chama cha Walimu Tanzania(CWT) kikitarajia kufanya uchaguzi wa viongozi wake wa kitaifa mwaka huu. Mmoja wa walimu wa shule ya sekondari Nambilanje, mkoani Lindi, Regimus Lilai leo ametangaza nia ya kugombea urais wa chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Lindi, Lilai alisema baaada ya kusoma na kuielewa katiba ya chama hicho amebaini kwamba anaweza na anahaki ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi ndani ya chama hicho cha wafanyakazi chenye wanachama wengi hapa nchini.

Alisema miongoni mwa sababu zilizomsukuma kugombea nafasi hiyo ya juu ya uongozi ni kutatua changamoto nyingi zilizopo kwenye chama hicho, ambazo zinasababisha vilio vya wanachama wake miaka nenda miaka rudi.

Lilai alizitaja baadhi ya changamoto hizo ambazo nisehemu ya vipaumbele vyake kuwa ni kukosekana kwa utawala bora. Hali inayosababisha wanachama kutoshirikishwa katika mambo yanayohusu chama chao. Ikiwemo kutosomewa taarifa za mapato na matumizi.

Japokuwa kina vitega uchumi, miradi na kunachukua ada za wanachama.

Aliitaja changamoto nyingine kuwa ni katiba ya chama hicho kutokuwa na kifungu kinachowapa uwezo wanachama  kuwaondoa viongozi waliotenda makosa na kushindwa kutekeleza wajibu wao.

 Maana yake nikwamba viongozi wa aina hiyo wanaendelea kuwa madarakani hadi wakati wa uchaguzi. Kitendo ambacho Lilai anaona ni kuwanyima haki na uhuru wanachama.

'' Chama hiki kina vitega uchumi na miradi mbalimbali. Nia ilikuwa ni kupunguza ukali wa maisha ya wanachama wake. Lakini licha ya walimu kukatwa asilimia mbili ya mishahara yao kila mwezi lakini hawanufaiki  na chochote,'' alisema Lilai.

Mwalimu huyo alikwenda mbali zaidi kwa kuwashangaa viongozi wa kitaifa wa CWT kwa kitendo cha kudai serikali ipungeze kiwango cha kodi kwa wafanyakazi lakini viongozi hao hawataki kupunguza kiwango cha ada ya wanachama wake inayokusanya kila mwezi. Licha ya kilio cha muda mrefu cha wanachama kuhusu kiwango hicho.

"Siyo vibaya kupigania maslahi ya walimu kwani hata mimi nikichaguliwa nitaendeleza madai hayo kwa serikali. Lakini iweje wenyewe wasianze kuonesha huruma kwa wanachama wake, badala yake wanaishupalia serikali tu?,'' alihoji.

Mgombea na Rais mtarajiwa huyo kijana alitoa wito kwa wagombea wote wanafasi hiyo wasipoteze fedha zao kuzunguka nchini kufanya kampeni za chini chini.

Bali uitishwe mdahalo ili kila mgombea aeleze mikakati na mipango yake na wanachama wawaulize maswali.

Post a Comment

0 Comments