Jinsi majasusi wanavyohangaika kuiba siri za chanjo ya corona

Majasusi ncini Marekani wanaripoti kuona taasisi za kijasusi za nchi nyingine wakijaribu kupitia mtandao kuchunguza tafiti za chanjo ya virusi vya corona nchini humo.
Mkurugenzi wa Kituo cha Ulinzi na Kukabiliana na Ujasusi wa Kimataifa cha Marekani Bill Evanina, ameiambia BBC kuwa serikali ya nchi hiyo tayari imeshatoa onyo kwa vituo vya utafiti wa kitabibu juu ya hatari ya kijasusi iliyopo.
Hata hivyo hakubainisha kama kumetokea wizi wowote wa taarifa kuhusu maendeleo ya tafiti za chanjo.
Vyanzo vetu vya usalama nchini Uingereza pia vimetuambia kuwa vimeona majaribio hayo ya kijasusi yakitokea.

Mashindano ya kutafuta chanjo

Kwa sasa kuna mbio za kimataifa zinazoendelea katika kutafuta kinga ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.
Watafiti, makampuni binafsi na serikali mbali mbali zinashiriki katika kutafuta chanjo. Na juhudi zao zinalindwa na taasisi za kijasusi za mataifa hayo, huku zikiwa zinalengwa na mashirika ya kijasusi ya nchi nyengine.
Kituo kinachoongozwa na Bwana Evanina kinatoa ushauri kwa serikali ya Marekani, makampuni na wasomi juu ya namna ya kujilinda na mashambulizi kutoka katika taasisi za kijasusi za nchi nyengine.
"Tumekuwa tukifanya kazi kwa karibu na watu kutoka serikalini na makampuni ili kuhakikisha tafiti zote na taarifa zake zinalindwa vilivyo," amesema.
"Tunatarajia kuwa taasisi za kijasusi za kigeni, pamoja na Chama Cha Kikomunisti cha Uchina, watajaribu kupata kile tukifanyacho hapa."
Serikali ya Marekani inajaribu kusaidia shughuli za utafiti kwa kuandaa operesheni maalumu.
Nchi yoyote ambayo itakuwa ya kwanza kupata chanjo salama na inayofanya kazi kwa ufanisi itawawezesha wananchi wake awali kufaidika na kuwa salama.
"Tumekuwa tukiwasiliana na kila taasisi ya utafiti wa matibabu ili wachukue hatua zaidi za kujilinda," ameeleza Bw Evanina.
"Katika dunia ya leo hakuna kitu cha muhimu kuiba kama taarifa za kitafiti ambazo zitakusaidia kupata kinga dhidi ya virusi vya corona."

Mashambulio dhidi ya hospitali

Katikati ya Mwezi Aprili, kachero mmoja mwandamizi wa FBI alisema kuwa kumekuwa na mashambulio ya kimtandao kwa baadhi ya taasisi ambazo zinashiriki katika tafiti zinazohusiana na corona.
Naibu mkurugenzi msaidizi w FBI Tonya Ugoretz alieleza kuwa taarifa za kitafiti za kimatibabu kwa kipindi kirefu zimekuwa "kipaumbele cha ujasusi wa kimtandao" na taasisi zinazofanya utafiti wa virusi zimekuwa zikilengwa.
Siku chache baadae, mwanasheria mkuu msaidizi wa usalama wa nchi, John Demers, alisema itakuwa ni "upuuzi wa hali ya juu" kufikiri kuwa Uchina hawatakuwa na haja na taarifa hizi. Taasisi ya Canada ya Usalama wa Mitandaoni ilitoa onyo mwezi Machi kuwa "kuna hatari ya majasusi mtandaoni ambao wanaweza kujaribu kuiba taarifa za kitafiti kutoka kwenye taasisi zinazofanya utafiti na maendeleo ya Covid-19."
Majasusi wa Marekani na nchi nyengine za Magharibi pia wanaweza kuwa na shauku ya kutaka kujua nini kinaendelea nchini Uchina pamoja na kutorandana kwa taarifa hususani za idadi ya vifo vilivyotokana na Covid-19 pamoja na tafiti za chanjo na matibabu.
Pia kumekuwa na hofu ya mashambulio ya kimtandao dhidi ya taasisi za afya, hali amabayo inaweza kudumaza uwezo wao wa kupambana na milipuko ya magonjwa.
Hospitali mbili ziliripoti mashambulizi ya mtandao Jamuhuri ya Czech mwezi Aprili.
Mashambulizi hayo yakasabisha Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo kutoa wito ambao si wa kawaida.
"Tunawataka wale ambao wamehusika kuacha mashambulizi ya kimtandao ya kutibua mfumo wa utoaji huduma za afya nchini Czech ama katika nchi nyengine yeyote ile," alieleza Pompeo katika taarifa yake.

Post a Comment

0 Comments