tangazo

Kansela Merkel, Papa Francis wasisitiza umuhimu wa kuzisaidia nchi maskini

 Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis wamezungumza kwa njia ya simu jana na kukubaliana juu ya umuhimu wa kuyasaidia mataifa masikini dhidi ya athari za virusi vya corona.

Msemaji wa ofisi ya Kansela amesema mazungumzo ya Bibi Merkel na Papa Francis yaligusia pia hali kisiasa na kiutu pamoja na umuhimu wa kuwepo mshikamano barani Ulaya na ulimwenguni kote dhidi ya mzozo wa COVID-19.

Kadhalika wakati wa mazungumzo hayo Kansela Merkel amemualika Papa Francis kuitembelea Ujerumani pindi kadhia ya virusi vya corona itakapomalizika.

Mazungumzo kati ya viongozi hao wawili yamefanyika siku moja baada ya Kansela Merkel kutangaza mipango ya Ujerumani ya kuondoa vizuizi kadhaa vilivyowekwa kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona na kuruhusu shughuli za kawaida kuanza kurejea polepole.

Post a Comment

0 Comments