tangazo

Kawawa aitaka Chalinze kudhibiti mapato

MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani Zaynabu Kawawa, amewataka viongozi wa Halmashauri ya Chalinze kutowafumbia macho watumishi wanaosababisha kushuka kwa mapato.

Aidha Kawawa amewakumbushia viongozi hao suala la kuwaweka watumishi wanaosimamia ushuru kukaa kwenye maeneo ya Makampuni yanayochimba kokoto, hatua inayolenga kuwadhibiti wafanyabiashara wanaojihusisha na ukwepaji wa ushuru.

Mkuu huyo alitoa kauli hiyo katika kikao cha kupitia taarifa ya Mkaguzi wa Serikali (CAG), kilichofanyika shule ya sekondari ya Lugoba, ambapo Halmashauri hiyo imepata hati safi kwa miaka minne mfululizo.

"Halmashauri ya Chalinze imekuwa kinara kwenye ukusanyaji wa ushuru, lakini nashangaa kwa nini hivi sasa mmeshuka kiasi hiki, Mwenyekiti na viongozi wenzako mlisimamie ili, na yeyote atayezembea katika kitengo hicho aondoke mwenyewe," alisema Kawawa.

Akizungumzia utekelezaji wa miradi ya Halmashauri kwa miaka minne mfululizo, Mwenyekiti Said Zikatimu alisema kuwa wamejenga shule mpya 4 za Sekondari, zahanati 39, wamegawa pikipiki kwa maofisa wa kilimo, mifugo na watendaji wa Kata, lengo kuboresha majukumu yao

"Shule za sekondari tulizozijenga ni Pera, Lupungwi, Chahua na ya Chamakweza ambayo tumeipeleka pesa kwa ajili ya kumalizia ujenzi wake, sanji na kupeleka pesa za kujenga majosho ya kuogeshea mifugo katika kila Kata," alisema Zikatimu.

Taarifa ya Ofisa Mkaguzi wa ndani Consolata Kiria, imeelezea kuwa utekelezaji wa mapendekezo ya hoja yaliyotolewa kwa mwaka 2018/2019 kuishia Juni 29 yalikuwa 44, yaliyotekelezwa na hoja kufungwa 18 sawa na asilimia 41, yanayoendelea kufanyiwakazi kulingana na maoni ya Mkaguzi yapo 26 sawa na asilimia 59.

"Mheshimiwa Mwenyekiti Halmashauri yetu kulingana na taarifa ya Mkaguzi wa Serikali, tumeendelea kupata hati safi kwa mwaka wa nne mfululizo, hii inatokana na kuendelea vizuri kwa utekelezaji wa shughuli za kimaendeleo kwenye Halmashauri yetu," ilimalizia taarifa hiyo.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Wilaya, Kaimu Mkurugenzi Zaynab Makwinya alisema kuwa kikao hicho cha kupitia taarifa ya Mkaguzi, kinalwnga kupitia utekelezaji wa kazi ndani ya halmashauru hiyo.

Akitoa shukrani kwa Mkuu wa wilaya kwa niaba ha Halmashauri hiyo, diwani wa Kata ya Kimamge Hussein Hading'oka alimpongeza Kawawa kwa usimamizi mzuri, na kwamba kutokana na kazi hiyo wamefanikiwa kutekeleza miradi ndio maana wamekuwa na hati safi katika kipindi chote

ADVERTISEMENT

Post a Comment

0 Comments