tangazo

Kenya yaitaka Somalia ichunguze 'kuanguka' ndege ya misaada ya corona

Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya imetaka uchunguzi wa haraka ufanyike baada ya ndege iliyobeba misaada ya kukabiliana na corona kuanguka kusini mwa Somalia, na watu wote sita waliokuwa ndani yake kufariki.

Ndege hiyo binafsi ilikuwa imebeba misaada ya kibinadamu inayohusiana na janga la corona wakati ilipoanguka ilipokuwa ikikaribia kutua katika uwanja wa ndege wa Wilaya ya Bardale kusini mwa Somalia yapata kilomita 300  kaskazini magharibu mwa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Katika tukio hilo, marubani wawili raia wa Kenya walipoteza maisha pamoja na raia wengine wanne wa Somalia. Wakuu wa Somalia wanasema uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo unaendelea.

Wizara ya mambo ya nje ya Kenya imetoa taarifa ikisema serikali ya nchi hiyo inaitaka Somalia kufanya uchunguzi wa haraka na wa kina kufahamu chanzo cha tukio hilo, na kuonya kuwa linaweza kuathiri mIsaada ya kibinadamu inayopelekwa nchini Somalia.

Affisa wa polisi katika eneo hilo Abdullahi Isack ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, "ndege hiyo ilikuwa inakaribia kutua katika uwanje mdogo wa ndege wa Bardale wakati ilipoanguka na kuteketea moto. Watu wote sita waliokuwamo walifariki."

Amesema bado haijabainika chanzo hasa cha ndege hiyo kuanguka huku akisisitiza kuwa uchunguzi unaendelea.
Naye Ahmed Isaq, afisa wa utawala katika eneo hilo ameliambia shirika la habari la AP kuwa roketi iliyofyatuliwa kutoka nchi kavu ililenga ndege hiyo wakati inakaribia uwanja wa ndege.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya imezitaka ndege za Kenya na za mashirika mengina ya kutoa misaada ya kibinadamu kuchukua tahadhari zikiwa katika eneo hilo kwa kuzingatia kuwa ndege hiyo imeanguka katika mazingira ya kutatanisha.

Kundi la kigaidi la al-Shabab linaendesha harakati zake kusini mwa Somalia lakini ndege hiyo imeanguka katika eneo linalodhibitiwa na wanajeshi wa serikali ya Somalia na pia askari wa Ethiopia.

Ndege iliyoanguka ni aina ya Embraer 120 na inamilikiwa na shirika la ndege la African Express la nchini Kenya.

Post a Comment

0 Comments