tangazo

Makampuni Yasaidia Mavazi ya Watoa Huduma

KAMPUNI ya Qwi - haya General Enterprises na Asas Group zimetoa msaada wa mavazi maalumu (coverall) ambayo ni sehemu ya mavazi ya watoa huduma (PPE) ili kuwasaidia watoa huduma katika vituo vya huduma za afya mkoani Iringa kujikinga wakati wakiwahudumia wagonjwa wenye maambukizi ya virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid- 19.

Msaada huo ni sehemu wa vifaa mbalimbali vya kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo vilivyotolewa juzi na taasisi tano kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Hapi ili kukabiliana na janga hilo mkoani Iringa.

Wakati kampuni ya Q wihaya imetoa mavazi 20, vitakasa mikono lita 75, sabuni za maji lita 100, vipima joto sita, barakoa na tangi kubwa za kunawia maji 62,vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh Milioni 12, Kampuni ya Asas Group imetoa msaada wa mavazi 40, barakoa 1,200, dawa na vifaatiba vyenye thamani ya Sh milioni 9.8.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo, Mkurugenzi wa kampuni ya Q wihaya Gerenal Enterprises, Leonard Mhenda alisema wametoa misaada hiyo wakiitikia wito wa serikali pamoja na miongozi iliyotolewa na Shirika la Afya Dunia (WHO) ya kuchukua hatua mbalimbali ili kujikinga na kuwakinga wengine wengine na maambukizi ya virusi vya Covid-19.

Akipokea misaada hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Hapi aliwataka wananchi kutoa taarifa za watu wote wenye dalili za ugonjwa huo kuwahi kwenye vituo vya kutolea huduma.

Mkuu wa mkoa alisema ugonjwa huo tayari umeingia mkoani Iringa na kwa taarifa ya wizara ya afya, maendeleo, jinsia, wazee na watoto kuna mtu mmoja aliyebainika kuwa na virusi hivyo baada ya kuingia mjini Iringa akitokea Dar es Salaam na alifariki Aprili 19, mwaka huu.

Alisema bado kuna watu wanasafiri bila sababu za msingi kwenda mikoa iliyoathirika sana na wengine wanakimbia mikoa iliyoathirika wanarudi Iringa. Akiwashukuru wadau wote wanaounga mkono mapambano ya kutokomeza ugonjwa huo kwa kutoa misaada ya vifaa na vifaa tiba, Hapi aliwataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu.

“Baadhi ya kinga ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya COVID 19 vinavyosababisha homa ya Corona ni pamoja na kuepuka msongamano, kunawa mikono vizuri kwa maji safi titirika na sabuni au maji yenye dawa, kutumia vitakasa mikono, kutumia barakoa, kuepuka kugusana na kukaa mbalimbali,” alisema.

Taasisi zingine zilizotoa msaada wa vifaa vya kujikinga ni pamoja na SAI Energy ya mjini Iringa iliyotoa katoni 15 za vitakasa mikono zenye thamani ya Sh 750,000 na taasisi ya Clinton iliyotoa vipima joto saba, barakoa 120, mavazi mawili na karatasi zenye matangazo 300.

Nyingine ni taasisi ya MOH ya mjini Dodoma iliyotoa vipima joto viwili, barakoa za kitiba zinazovaliwa na matabibu wakati wa upasuaji 4,000 na mavazi maalumu ya watoa huduma 35.

Post a Comment

0 Comments