tangazo

Marais wa Kenya na Somalia waafiki uchunguzi wa pamoja kuhusu ajali ya ndege

Marais wa Kenya na Somalia wamekubaliana kufanya uchunguzi wa pamoja kuhusu ajali ya ndege iliyotokea Jumatatu eneo la Bay nchini Somalia na kusababisha vifo vya watu sita.

Rais wa Somalia Mohamed Farmaajo amempigia simu Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na kubainisha masikitiko yake kufuatia ajali hiyo na kuongeza kuwa  Mamlaka ya Usafiri wa Anga Somalia imeanzisha mara moja uchunguzi kuhusu ajali ya ndege hiyo, ambayo hutoa huduma za kuunga mkono shughuli za kibinadamu. Aidha Rais Farmojo ameialika Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Kenya (KCAA) kushirikiana na wenzao wa Somalia kwa lengo la kukamilisha uchunguzi haraka.

Rais Uhuru Kenyatta amemshukuru Rais Farmaajo kwa simu yake na amesema atazifikishia familia za marubani wawili wa Kenya salamu za rambi rambi.

Ndege hiyo ya binafsi ilikuwa imebeba misaada ya kibinadamu inayohusiana na janga la corona wakati ilipoanguka ilipokuwa ikikaribia kutua katika uwanja wa ndege wa Wilaya ya Bardale kusini mwa Somalia yapata kilomita 300  kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa Somalia,


Katika tukio hilo, marubani wawili raia wa Kenya walipoteza maisha pamoja na raia wengine wanne wa Somalia. Wakuu wa Somalia wanasema uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo unaendelea.

Walioshuhudia tukio hilo wanasema kuwa roketi iliyofyatuliwa kutoka nchi kavu ililenga ndege hiyo wakati inakaribia uwanja wa ndege.

Ndege iliyoanguka ni aina ya Embraer 120 na inamilikiwa na shirika la ndege la African Express la nchini Kenya.

Kundi la kigaidi la al-Shabab linaendesha harakati zake kusini mwa Somalia lakini ndege hiyo ilianguka katika eneo linalodhibitiwa na wanajeshi wa serikali ya Somalia na pia askari wa Ethiopia.

Post a Comment

0 Comments