tangazo

Ningekua Spika wa bunge ningewacharaza bakora wabunge wa upinzani walioondoka bungeni - RC Chalamila

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, amesema angekuwa Spika wa Bunge, angewacharaza bakora wabunge wa vyama vya upinzani waliotoka Bungeni wakishinikiza vikao vya Bunge viahirishwe kutokana na tishio la ugonjwa wa Corona.

Chalamila ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa anazungumza kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo cha kupokea na kujadili hoja zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambapo amesema hoja za wabunge hao ni za kitoto.

Amesema wabunge hao ni wa ajabu kwa sababu walikubaliana kukacha vikao vya Bunge kwa sababu ya kuogopa corona huku wakitaka Bunge lijadili na kupitisha bajeti ya dharura kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo.

"Simfundishi Spika kazi lakini ningekuwa mimi ndio Spika, ningepitisha viboko mle bungeni mpaka wakome maana hoja zao ni za kitoto, sasa hiyo bajeti ya dharura walitaka ijadiliwe wapi kama wanakacha vikao?" amesema Chalamila.

Chalamila amesisitiza kuwa kitendo cha wabunge hao kukacha vikao vya bajeti huku wakitaka Bunge hilo kujadili bajeti ya dharura ni kuwachanganya wananchi.

Amewataka madiwani wa Halmashauri zote za Mkoa huo bila kujali itikadi za vyama vyao kuungana na kufanya kazi kwa bidii badala ya kukacha vikao kama walivyofanya wabunge wa vyama vya upinzani.

Hata hivyo Chalamila amewataka watanzania kuwapuuza watu wote wanaotaka watu kujifungia ndani (Lockdown) kwa maelezo kuwa watanzania hawana uchumi wa kuwawezesha kutekeleza jambo hilo pamoja na uwepo wa janga la Corona.

Amewataka watanzania kuendelea kufanya shughuli zao za kiuchumi huku wakichukua tahadhari ya maambukizi ya Corona na kuwapuuza wapotoshaji.

Aidha, Chalamila amewapongeza madiwani na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe kwa kushirikiana kusimamia mapato na kuifanya Halmashauri hiyo kuondokana na hati yenye mashaka ambayo aliipata katika Mwaka wa fedha 2017/2019.

Amewataka watendaji wa Halmashauri hiyo kwa kushirikiana na madiwani kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato na kusimamia vizuri vyanzo hivyo ili kuongeza makusanyo.

Awali akifungua Kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Ezekiel Mwakota, amesema Halmashauri hiyo imepata hati ya kuridhisha kutokana na ushirikiano walioupata kutoka  kwa viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Mariam Mtunguja ambaye amekuwa anawashauri kuhusu usimamizi wa fedha.

"Baada ya kupata hati yenye mashaka mwaka wa fedha uliopita, tulikaa chini na kuanza kufanyia kazi dosari zilizokuwepo na kuongeza ushirikiano ambao umetusaidia kupata hati hii ya kuridhisha," amesema Mwakota.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Rungwe amesema Halmashauri inapopata hati chafu au yenye mashaka wanaochafuka ni viongozi wote wa Wilaya pamoja na Mkoa kwa maelezo kuwa wanakuwa hawajazisimamia vizuri Halmashauri husika.

Amesema ataendelea kuzishauri Halmashauri zote za Wilaya hiyo kusimamia ukusanyaji wa mapato na matumizi sahihi ya fedha hizo ili kuepuka hati chafu na ambazo haziridhishi.

Post a Comment

0 Comments