Serikali yaahidi kuongezea mtaji Benki ya TADB, yaipongeza kwa kuwainua wawekezaji wadogo


SERIKALI imeahidi kuiongezea mtaji Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kutokana na namna inavyowasaidia wakulima na kuwapa kipaumbele wawekezaji wazawa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angela Kairuki leo wilayani Manyoni, Singida wakati alipofanya ziara ya kutembelea kiwanda cha kuchakata mbegu za Alizeti cha Qstek.

Akizungumza kiwandani hapo, Waziri Kairuki ameipongeza Benki ya Kilimo kwa namna ambavyo imekua ikiwainua wakulima na wawekezaji wadogo tofauti na Taasisi zingine za fedha.

Ameipongeza benki hiyo kwa kuwapatia wawekezaji hao wa Qstek kiasi cha Sh Bilioni 2.2 kwa ajili ya uwekezaji wa kiwanda hiko ambacho kitakua na uwezo wa kuchakata mbegu za alizeti tani 6,000 kwa mwaka na kuzalisha mafuta ya kula yenye ubora tani 2,500 kwa mwaka.

" Niwapongeze TADB kwa namna mnavyowashika mkono wakulima, mtaji wa Bilioni 2.2 mlioutoa hapa ni mkubwa sana, niwasihi muendelee kuwawezesha zaidi hadi watakaposimama kabisa. Nafahamu pia mmewezesha wakulima 829 na mna mpango wa kuwawezesha wengine Laki mbili. Hongereni sana.

Onesheni mfano wa kusaidia wakulima na vijana wetu ili kwa pamoja tuweze kufikia malengo na ndoto ya Rais wetu ifikapo mwaka 2025 ya kuwa na uchumi wa kati unaotegemea viwanda," Amesema Kairuki.

Amesema serikali imeweka unafuu wa kikodi kwa wawekezaji nchini ili kuvutia uwekezaji na kuwataka wakurugenzi wa Halmashauri nchini kutenga maeneo ya uwekezaji na wasiwakwamishe wawekezaji wanaotaka kuwekeza viwanda na miradi mbalimbali.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Benki ya TADB, Japhet Justine amesema mpaka sasa ujenzi wa mradi huo umegharimu Sh Bilioni tatu huku wao kama wadau wa maendeleo wametoa kiasi cha Sh Bilioni 1.5 kwa ajili ya kusaidia gharama za ujenzi wa majengo ya kiwanda na Sh Milioni 718 kwa ajili ya kusaidia kuanzisha uzalishaji.

Justine amesema Tanzania kwa viwanda vya mafuta vilivyopo inazalisha tani 201,0000 lakini bado haitoshi na kuongeza kuwa njia pekee ya kufanya Mapinduzi katika sekta ya mafuta ni kuwezesha wakulima wadogowadogo kufanya kilimo cha kisasa.

" Tunapaswa kuwasaidia wakulima wadogo wadogo na sisi kama Benki ya Maendeleo ya Kilimo tumeshaanza kuchukua hatua ya kuhakikisha wakulima hawa wanahama kutoka kwenye ule mfumo wa kutumia mbegu ambazo walizitumia mwaka jana na msimu mpya ukianza wanazitumia tena, tayari tushaanza kufanyia kazi hilo.

Tunaamini tukihamasisha kuwainua wakulima wadogo wadogo tutawainua wengi hapa Manyoni na sehemu zingine nchini, kwahiyo Mhe Waziri nikuahidi tutaendelea kushirikiana na Mkoa wa Singida katika kuwainua wakulima wa Alizeti ambao tunaamini wakiinuka wao na Singida imenyanyuka," Amesema Justine.

Justine amesema huu ni mkopo wao wa pili ndani ya Mkoa wa Singida ambapo tayari wameshatoa zaidi ya Milioni 600 kwa wakulima wadogo wadogo waliokua wanazalisha alizeti pamoja na hizo Bilioni 2.2 kwa ajili ya kiwanda hiko cha Qstek lengo ni kuhakikisha Tanzania inakua Nchi inayoongoza kwa kuuza mafuta ya alizeti nje ya Nchi.

Nae Mkurugenzi wa Kiwanda hiko, Emmanuel Nagunwa ameishukuru Serikali kwa kuwawezesha kuanzisha kiwanda hiko ambacho kitaongeza wigo wa biashara ya zao la alizeti na kuchochea mapato kupitia kodi mbalimbali zinazotokana na uzalishaji wa kiwanda hiko.

Amesema kiwanda kinatarajia kutoa ajira za moja kwa moja zipatazo 70 na ajira zisizo rasmi 100 na pia kitaleta tija za kiuchumi katika Wilaya ya Manyoni ambapo wakulima wa zao la alizeti mkoa wa Singida na mikoa jirani watapata soko la uhakika kwa kuuza mazao baada ya kuvuna.

" Niishukuru sana Benki hii ya TADB kwa hakika imekua msaada mkubwa kwetu katika kufikia malengo yetu, wametusaidia kwa kiwango kikubwa kutuwezesha mtaji na fedha za ujenzi, tunaamini kiwanda chetu kitakua chachu ya mafanikio na maendeleo ya wilaya yetu," Amesema Nagunwa..

Kiwanda hiko kimefikia hatua ya mwisho na kinatarajiwa kuanza uzalishaji wake kuanzia mwezi Agosti mwaka huu.

Post a Comment

0 Comments