tangazo

Shilingi 103.8 bilioni kugharamia usambazaji umeme wa gharama nafuu mitaa ya mijini


Katika kuhakikisha wananchi wanaoishi mitaa ya mijini ambayo inafanana na vijiji wanapata umeme wa gharama nafuu. Serikali imetenga shilingi 103,800,000,000(103.8 bilioni) kwa ajili ya kusambaza nishati hiyo katika mitaa ya mijini. Hayo yameelezwa na waziri wa nishati, Dkt Menrad Kalemani wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia kwa wateja wa nishati ya kupikia majumbani. Hafla ambayo ilifanyika jana katika mtaa wa Mnazi Mmoja, manispaa ya Lindi


Dkt Kalemani alisema serikali imetenga kiasi hicho cha fedha ili wananchi wengi wanaoishi katika mitaa ya mijini ambayo mazingira yake yanafanana na vijiji wapate umeme wa gharama nafuu. Ambapo gharama za kuunganishiwa umeme huo itakuwa sawa na vijijini ambayo ni shilingi 27,000. Kutokana na azima hiyo ya serikali, waziri Kalemani amemuagiza meneja wa shirika la umeme(TANESCO) wa kanda ya Kusini ahakikishe utekelezaji wa azima huyo unaanza Julai, Mosi, mwaka huu wa 2020 katika mikoa ya Lindi na Mtwara. Alisema haoni tofauti kati ya baadhi ya mitaa ya mijini na vijijini. Kwahiyo hakuna sababu ya kuwa na tofauti ya gharama ya kuwaunganishia wateja wa mijini wa mitaa inayofanana na vijiji.

Kuhusu usambazaji wa gesi asilia kwa wateja wa majumbani, waziri Kalemani alisema gharama za kuunganisha kwa wateja inabebwa na serikali. Kwahiyo ameliagiza TPDC isiwatoze wateja, wananchi waanze kutumia nishati hiyo ndani ya miezi sita kuanzia sasa, isambazwe kwenye mitaa yote ya kata za Mingoyo, Kiwalala na Mnazi Mmoja na isambazwe na kuunganishwa kwenye nyumba za aina zote bila kubagua. Alibainisha kwamba mradi huo wa ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia majumbani utagharimu shilingi 28.8 bilioni ambazo zinatokana na mapato ya ndani ya nchi.

Waziri huyo alitoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Lindi watumie gesi asilia. Kwani matumizi ya kuni na mkaa gharama yake nikubwa. Lakini pia itapunguza uharibifu wa misitu na mazingira.

Post a Comment

0 Comments