Tathimini ya ununuzi wa pamba kufanyika kabla ya msimu

Serikali imesema inafanya tathmini ya hali ya ununuzi wa zao la pamba msimu wa mwaka 2019 ili kuondoa changamoto zilizojitokeza kabla msimu mpya wa ununuzi kuanza mwaka huu.

Akizungumza na viongozi wa wilaya ya Chato mara baada ya kutembelea viwanda vya kuchambua pamba, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amesema msimu mpya wa ununuzi utatangazwa mara baada ya tathmini ya msimu uliopita kufanyika.

“ Wizara imegundua kuwa hali ya mazao shambani kwa pamba bado ,kwani hata vitumba bado havijapasuka kutokana na uwepo mvua nyingi ,hivyo baada ya ziara hii kwenye mikoa ya kanda ya ziwa serikali itakaa na watalaam ili kuamua lini wakulima wataanza kuuza pamba yao kupitia Vyama Vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) “ alisema Kusaya.

Aliongeza kusema kabla msimu haujafunguliwa serikali itahakikisha madeni ya wakulima,wanunuzi na
ushuru wa AMCOS, halmashauri pamoja na mfuko wa pembejeo yanalipwa.

“Kila mwananchi atalipwa madai yake na jitihada za serikali ni kuona madeni haya yanalipwa kabla ya
msimu mpya wa ununuzi wa pamba kuanza” alisitiza Katibu mkuu.

Katika hatua nyingine Chama Kikuu cha Ushirika Chato( CCU) kimetakiwa kuhamasisha wakulima wengi
zaidi kuzalisha zao la pamba ili ipate malighafi za kutosha kutumika kwenye kiwanda chake cha
kuchambua pamba.

Kusaya alitoa wito huo kufuatia taarifa ya Meneja Mkuu wa Chama hicho Joseph Masingiri kusema kiwanda kimeshindwa kuendelea na uchakataji marobota kutokana na uhaba wa pamba ambapo msimu wa 2019 ni kilo milioni 13.6 ,000 tu zilinunuliwa wakati uwezo wake ni kilo milioni 30.

Ili kukabiliana na changamoto za zao hilo,Katibu Mkuu Kusaya amewataka wataalam wa halmashauri na
wa chama kikuu kuhamasisha wakulima kuzalisha mazao ya mkonge na korosho ili kuwa na uhakika wa
kipato pale zao la pamba linapoyumba.

“ Tulime pamba na mazao mengine ya biashara kama mkonge na korosho yanayostawi vizuri kwenye
mkoa huu wa Geita na kanda ya ziwa yote .Wizara ya kilimo ipo tayari kuleta mbegu bora za mkonge na
korosho toka taasisi za utafiti ili zigawiwe kwa wakulima “ Kusaya.

Kusaya alitaja faida za zao la mkonge kuwa katika kipindi cha miaka mitatu baada ya kupanda mkulima
ataanza kuvuna na kuendelea hadi miaka kumi na tano huku akiendelea na kilimo cha mazao mengine .

Katika kuhakikisha mkoa wa Geita unaongeza uzalishaji wa mazao nchini,Katibu Mkuu huyo ameelekeza
mkoa uwasilishe wizarani maandiko ya miradi ya kipaumbele ya umwagiliaji ili serikali itafute wadau wa
kuitekeleza.

Nae Katibu Tawala Mkoa wa Geita Dennis Bandisa aliyeshiriki ziara hiyo aliishukuru wizara ya kilimo kwa
kuonesha nia ya kusaidia kukuza kilimo cha umwagiliaji na kuwa kuahidi kuwa maandiko atayawasilisha
wizarani ndani ya kipindi kifupi.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Eliurd Mwaiteleke kuhusu sekta ya kilimo ilisema wilaya hiyo ina eneo la hekta 10,810 zinazofaa kwa umwagiliaj lakini ni hekta 3,416 tu sawa na asilimia 31.6 zinamwagiliwa.

Katika msimu wa mwaka 2019 jumla ya kilo milioni 10.8 za pamba mbegu zilinunuliwa wilayani Chato kupitia AMCOS zenye thamni ya shilingi Bilioni 13.06 ililipwa kwa wakulima.

Post a Comment

0 Comments