tangazo

Virusi vya Corona: Kikao cha bunge cha mtandaoni Afrika kusini chadukuliwa kwa picha za ngono

Spika Thandi Modise alisema kuwa yeye sio shabiki wa mikutano inayofanyika kwa njia ya Zoom mtandaoni

Mkutano wa kamati ya bunge kwa njia ya mtandao Afrika Kusini umevamiwa na wadukuzi na spika kudhalilishwa.

Kikao hicho kilikuwa tu ndio kimeanza Alhamisi asubuhi wakati ambapo picha za ngono zilipojitokeza kwenye skrini huku sauti ya mwanamume ikisikika kumtusi Spika Thandi Modise, ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho.

Spika huyo aliyeshikwa na hasira alipaza sauti akisema hiyo ndio sababu anapinga mikutano ya mitandaoni.

"Hiki kilichotokea ni kilekile nilichokuwa ninakisema kuhusu kufanya mikutano kwa njia ya Zoom!" Bi Modise amenukuliwa akisema hivyo na tovuti ya Times Live.

Wabunge walielezea tukio hilo kama lenye kukera na kutatiza akili, kulingana na Tovuti ya habari ya Eyewitness.

Iliwalazimu wahandisi wa Bunge kutuma kiunganishi chengine ambapo wabunge waliunganika tena na kuendelea na kikao chao.

Bunge la Afrika Kusini kwa sasa limefungwa na mikutano yote inafanyika kwa njia ya mtandaoni wakati ambapo nchi hiyo bado inatekeleza kanuni za kukabiliana na virusi vya corona.

Hii sio mara ya kwanza kwa tukio kama hilo kutokea kwasababu simu ya mbunge mmoja iliyokuwa inafanyika kwa njia ya video pia naye aliwahi kuvamiwa namna hiyo.

Kampuni ya mtandao wa Zoom imekuwa ikikosolewa kimataifa kwa taarifa kwamba kuna wavamizi wanaotuma picha za ngono au maudhui ya matusi wakati wa mikutano.

Kuvamiwa kwa mtandao kwa njia ya Zoom kumekuwa kukifanyika mara kwa mara katika wiki za hivi karibuni wakati ambapo watumiaji wengi wapya wameanza kutumia mtandao huo kama njia moja ya kukabiliana na kusambaa kwa ugonjwa wa Covid-19 na kuahirishwa kwa mikutano na matukio ambayo awali ilikuwa ifanyike ana kwa ana.

Post a Comment

0 Comments