WMO : Sehemu nyingi duniani kukabiliwa na joto lisilo la kawaida

Shirika la hali ya hewa duniani -WMO linasema sehemu nyingi za dunia zitarajie hali ya joto joto kuliko kiwango cha kawaida kutoka mwezi huu wa Mei hadi Juni 2020.
Shirika hilo linasema hii ni kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayo sababishwa na binadamu. WMO pia imetoa taarifa yake mpya ya msimu juu ya hali ya hewa.
Wanasayansi wa hali ya hewa wanatarajia kiwango cha juu cha joto katika muda wa miezi mitatu ijayo, licha ya kutokuwepo El Nino, janga la asili ambalo hutokea na kuongeza kiwango cha joto ulimwenguni.
Katika miaka iliyopita, kiwango cha joto kali kimetokea katika miaka ya El Nino. Lakini hilo linabadilika. Taasisi inayofuatilia hali ya hewa Duniani inasema kwamba mwezi April mwaka huu wa 2020, kipindi kisicho cha El Nino kimekutana na mwezi wa joto kali kwenye rekodi ya mwezi April mwaka 2016, wakati ambapo kulikuwa na El Nino kali sana Pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa.
Msemaji wa WMO, Claire Nullis anasema miaka yote hiyo hadi mwaka 2016 imekuwa na hali ya joto bila ya El Nino, ikiwemo mwaka 2019, ambao ulikuwa mwaka wa pili wenye hali ya joto sana katika rekodi. Anaeleza hali hiyo inaendelea hadi kuingia mwaka 2020.
Anaeleza : "Hali ya kiwango cha joto ulimwenguni katika mwezi Januari, Februari na Machi pia ilikuwa ya joto-joto au mwaka wa pili wenye hali ya joto katika rekodi, kulingana na takwimu zilizopo za kimataifa. Hivyo basi hivi sasa tunaona ushawishi wa binadamu una nguvu sana juu ya mabadiliko ya hali ya hewa."
WMO inasema matukio mengi yenye hali mbaya ya hewa yanatokea dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa. Inasema mawimbi ya joto yanaongezeka kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, na hilo linasababisha madhara makubwa kwenye matukio mabaya kama vile vimbunga na mvua kali. Afrika mashariki kwa mfano inashuhudia mvua nyingi na mafuriko.
Nullis ameiambia Sauti ya Amerika-VOA kwamba kujiandaa kwa hali hii na kudhibiti madhara ya matukio mabaya sana ya hali ya hewa inakuwa vigumu sana kutokana na janga la COVID-19. Anaeleza kwamba mataifa hayachukui hatua za kutosha kwa mifumo inayotoa onyo mapema kwa sababu ya janga hili.
"Kwa hakika tunahitaji njia mbali mbali mbadala za mifumo inayotoa onyo la mapema dhidi ya majanga, dhidi ya mawimbi ya joto kwa sababu vitu hivi vyote vinashabihiana. Vinaleta madhara na COVID hivi sasa ni moja ya vitu hivyo hatarishi," anasema mataalam huyo.
Wanasayansi wa WMO wanasema janga la COVID-19 ni zaidi ya janga jingine lililowahi kutokea hapo kabla, linaongeza umuhimu wa kuwepo utabiri wa hali ya hew ana mitazamo ya muda mrefu ya hali ya hewa. Wanasema viwango vya joto na unyevunyevu vina madhara makubwa kwenye masuala muhimu ya kiuchumi na mifumo ya afya ya umma, ikielezewa kwamba shughuli nyingi ziko katika hali ya kuanguka kutokana na janga hili.

Post a Comment

0 Comments