Bunge la Burundi laidhinisha uteuzi wa Makamu Rais, Waziri Mkuu

Jenerali Alain-Guillaume Bunyoni, Waziri mkuu mteule wa Burundi
Bunge la Burundi Jumanne liliidhinisha uteuzi wa makamu rais na waziri mkuu, ambao walipendekezwa na rais mpya, Evariste Ndayishimiye.
Prosper Bazombanza kutoka chama cha UPRONA aliidhinishwa kama makamu rais kwa kura 91, huku wabunge wawili wakikosa kumuunga mkono na mmoja mmoja kutopiga kura
Naye Alain-Guillaume Bunyoni, afisa mwenye cheo cha juu sana katika polisi ya taifa hilo, ambaye ni waziri wa usalama wa muda mrefu wa serekali inayoondoka madarakani, alipitishwa kwa jumla ya kura 94 za wabunge, kama Waziri mkuu mpya.
Cheo cha Waziri Mkuu ni kipya, kwa mujibu wa katiba mpya ya Burundi. Katiba hiyo pia imeondoa cheo cha mmoja wa makamu wa rais, kwani katiba ya zamani ilitambua makamu wawili wa rais.
Bazombanza aliwahi kuhudumu kama makamu wa kwanza wa rais chini ya uongozi wa rais wa zamani aliyefariki, Pierre Nkurunziza, kuanzia mwaka wa 2014 hadi 2015.
Bunyoni yupo chini ya vikwazo vya Marekani na umoja wa ulaya kwa tuhuma za ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, wakati wa maandamano ya April 2015, ya kupinga muhula wa tatu wa Rais Nkurunziza.
Wakati huo huo, habari ambazo hazijathibitishwa zinaeleza kwamba mwili wa rais wa zamani, Pierre Nkurunziza, utazikwa Ijumaa tarehe 26 katika mji wa Gitega, ulio takriban Kilomita sitini Mashariki mwa Bujumbura, kwa mujibu wa gazeti la New Times la Rwanda.
Nkurunziza alikufa kutokana na kile serikali ilisema ni "shinikizo la moyo" licha ya kuwepo kwa tetesi kwamba huenda alikufa kutokana na maambukizi ya Corona.

Post a Comment

0 Comments