Waziri wa nishati wa Mexico Rocio Nahle amesema jana kuwa nchi hiyo haitarefusha muda wa kupunguza uzalishaji wa mafuta, hatua iliyokubaliana na shirika la nchi zinazosafirisha mafuta kwa wingi duniani OPEC mnamo mwezi Aprili. Uamuzi huo unakuja baada ya Shirika hilo la OPEC na mataifa washirika wake kukubaliana jana kurefusha muda wa kupunguza uzalishaji wa mafuta wa takriban mapipa milioni 10 kwa siku ambao muda wa awali wa makubaliano hayo ulikuwa unakamilika mwezi Julai wakitumaini kuchochea udhibiti wa soko la mafuta ulioathirika kutokana na mzozo wa kiuchumi duniani unaotokana na janga la virusi vya corona. Mkutano huo uliofanyika kwa njia ya video kati ya wanachama wa OPEC na washirka wake wakiongozwa na Urusi, ulilenga kupunguza uzalishaji wa ziada wa mafuta hatua inayochangia kupungua kwa bei ya bidhaa hiyo huku ndege nyingi duniani zikikatiza shughuli zake kutokana na janga hilo. Punguzo hilo la uzalishaji linawakilisha asilimia 10 ya usambazaji wa jumla wa bidhaa hiyo ulimwenguni.
0 Comments