tangazo

Raheem Sterling aongelea vitendo vya kibaguzi baada ya kifo cha Floyd

 
Sterling amefunga magoli 12 katika michezo 56 ya England
Mshambuliaji wa England na Manchester City Raheem Sterling ameunga mkono maandamano yanayofanyika nchini Uingereza, akisema '' ugonjwa pekee kwa sasa ni ubaguzi tunaopambana nao''.
Maelfu ya watu wamefanya maandamano ya 'Black Lives Matter' nchini Uingereza, pamoja na maonyo yanayotolewa na serikali kuepuka mikusanyiko kwa sababu ya tishio la virusi vya corona.
''Hili ni jambo muhimu zaidi kwa wakati huu kwasababu ni jambo ambalo limekuwa likifanyika kwa miaka na miaka,'' alisema Sterling ,25 .
Maandamano makubwa yamefanyika jijini London, Bristol, Manchester, Wolverhamton, Nottingham, Glasgow na Edinburgh baada ya kifo cha Mmarekani mweusi, George Floyd.
Floyd, 46, alipotea maisha akiwa mikononi mwa polisi tarehe 25 mwezi Mei mjini Minneapolis. Maafisa wanne waliohusika na tukio hilo wameshtakiwa wakihusishwa na kifo chake, ambacho kiliibua maandamano nchini Marekani na maandamano sehemu nyingine duniani.
Akizungumza na kipindi cha Newsnight cha BBC, Sterling amesema: ''Kama ilivyo kwa janga hili, tunataka kupata suluhisho kukomesha vitendo hivi.
''Wakati huo huo, hiki ndicho waandamanaji wanachokifanya. Wanajaribu kupata suluhisho na namna ya kukomesha vitendo visivyo vya haki wanavyoviona .
''Kama wanafanya kwa amani na kwa usalama na bila kumdhuru yeyote na bila kuvunja maduka, wanaendelea kuandamana kwa amani.''
Wanamichezo wamezungumzia kifo cha Floyd, pia wachezaji wenzake Sterling wa timu ya England kama vile Jadon Sancho.
Raheem Sterling
Sterling, ambaye timu yake inarejea kwenye ligi ya primia tarehe 17 mwezi Juni amesmea ''Kwanza kabisa, kwa kweli sifikirii kazi yangu kwanza mambo kama haya yanapotokea. Huwa ninafikiri kilicho sahihi.
''Ninaendelea kusema neno hili. Ninawaona watu wengi kwenye mitandao ya kijamii wakiunga mkono suala hili. Lakini hili ni suala ambalo linahitaji zaidi ya kuongea tu.
''Tunahitaji kufanyia kazi suala la mabadiliko kuweka wazi maeneo yanayohitaji mabadiliko.
''Lakini hili ni jambo ambalo mimi mwenyewe nitaendelea kulifanya kuchochea mjadala na kuwafanya watu wafikirie jambo la kufanya ili kuwapa watu nafasi sawa kwenye nchi hii.
''Nina matumaini kuwa na watu wa tasnia nyingine wanaweza kufanya hivyo pia.''
Mcheza kriketi wa England Jofra Archer amsema matukio ya wiki moja iliyopita yanaonesha ''jinsi watu ulimwenguni kote wanavyounga mkono usawa''.
Mchezaji huyo wa miaka 25 alishawahi kuoneshwa vitendo vya ubaguzi wa rangi.
''Watu hawatanyamaza kimya na kuacha vitu tu vikifanyika,'' Archer aliandika katika safu yake ya Daily Mail.

Post a Comment

0 Comments