tangazo

Ripoti ya UNESCO:Robo milioni ya watoto duniani wakosa elimu

Ripoti mpya ya hali ya elimu duniani ya shirika la Umoja wa Mataifa, UNESCO imesema karibu watoto milioni 258 hawakwenda shule mnamo mwaka 2018. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 17 ya vijana ulimwenguni kote.
Kulingana na makadirio ya shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO, takriban asilimia 90 ya vijana walioathiriwa zaidi ni kutoka katika nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara na Asia. Umasikini umetajwa kuwa ndio haswa unaoathiri fursa za elimu.
Ripoti hiyo pia imeeleza kwamba mamilioni ya wavulana na wasichana wanabaguliwa katika mifumo ya elimu kwa sababu ya asili zao au ulemavu walionao. Mkurugenzi Mkuu wa Unesco Audrey Azoulay amesema janga la corona limeathiri zaidi shughuli za elimu na kwamba tatizo hilo la kiafya linaweza kuwa chanzo cha kuwafanya watoto wengi wasirudi shuleni hasa wasichana kutoka familia masikini.
Ripoti hiyo ya UNESCO imebaini kuwa katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, watoto wenye ulemavu, kwa asilimia 19 wapo chini ya kiwango cha kuhudhuria masomo na kwamba katika mataifa 20 masikini, barani Afrika yaliyo Kusini mwa Jangwa la Sahara, wengi wa wasichana wa vijijini hawapati elimu ya shule ya sekondari.
UNESCO imesema kwenye ripoti yake kwamba kwa bahati mbaya, makundi yenye matatizo mbalimbali yanawekwa au yanasukumwa nje ya mifumo ya elimu kupitia maamuzi ambayo yanasababisha kutengwa  kimitaala, malengo yasiyofaa katika ufundishaji, vitabu vinavyotumiwa, ubaguzi katika ugawaji wa rasilimali, vurugu na hata kupuuzwa kwa mahitaji ya wanafunzi.

Post a Comment

0 Comments