Saudi Arabia, Umoja wa Mataifa waitisha mkutano wa ufadhili kwa Yemen

Umoja wa Mataifa na Saudi Arabia zimeshirikiana kuitisha mkutano wa wafadhili kwa njia ya mtandao wakidhamiria kukusanya zaidi ya dola bilioni 2 kuisaidia Yemen, taifa lililokumbwa na ufukara, mauaji, na sasa COVID-19.
Ukienda kwenye soko kuu la Sanaa, unakutana na nguo za kila rangi, vitabu vikongwe, tani kwa tani za peremende, na pirika za ngia-toka kama kwamba hakuna kinachoendelea.
Watu hapa wanabanana kwenye mitaa myembaba, wakisimama karibu sana na washitiri, wakipatana bei za bidhaa. Si rahisi hapa kuweka  masafa ya mita moja na nusu baina ya mtu na mtu.

"Bila shaka, tunaogopa. Lakini nalazimika kutoka kununuwa mahitaji ya wanangu. Naogopa lakini sina budi kuja kununuwa mahitaji muhimu. Tunatarajia dunia inatuona na inafahamu kuwa sisi Wayemeni tupo mitaani lakini pia tunaogopa virusi vya korona vinavyouwa," anasema Qaboos Bin Said Al Houkaly, mmoja ya wale wachache waliovaa barakowa kwenye soko hili.
Mwanzoni mwa mwezi Aprili, mtu wa kwanza aligundulika na virusi vya korona nchini Yemen na tangu hapo, kumekuwa na wasiwasi mkubwa kwamba idadi ya walioambukizwa inapanda, katika nchi ambayo tayari mamilioni wanatapatapa angalau waweze kuishi siku yao moja.

Hata kabla ya korona, Yemen ilishakuwa taabani

Kumekuwa na vita kati ya Wahouthi, kabila la watu wa kaskazini mwa nchi hiyo, na Saudi Arabia, ambayo inaunga mkono serikali inayotambuliwa kimataifa lakini isiyo na nguvu. Huu ni mwaka wa tano sasa.


Post a Comment

0 Comments