Serikali yatoa hatua zinazofuata kwenye Tanzanite

Waziri wa Madini Dotto Biteko amesema serikali itakuja na mpango wa namna ya matumizi ya mawe ya madini ya Tanzanite yaliyopatikana Mererani, ambayo yameweka rekodi ya kuwa makubwa zaidi katika historia ya uchimbwaji wa madini hayo.


Waziri wa Madini Dotto Biteko akiwa na mchimbaji mdogo Saniniu Laizer wilayani Simanjiro mkoani Manyara.

Akiongea kupitia Supa Breakfast ya East Africa Radio, Biteko amesema kwa kuwa madini hayo yamenunuliwa na serikali hivyo hata utaratibu wa kuyatumia utawekwa wazi hivi karibuni.

''Serikali itakuja na utaratibu wa namna gani mawe hayo yatatumika au kama ni kuwekwa kwenye makumbusho yetu bahati nzuri haya mawe yanamilikiwa na serikali hivyo utawekwa utaratibu na mtaelezwa hapo baadaye'', amesema.

Aidha Dotto Biteko amesema, ''Pesa inayopatikana kupitia uchimbaji wa madini ya Tanzanite kwasasa inafikia mpaka Bilioni 50, hivyo mapato ya serikali nayo yamepanda kutoka Shilingi Milioni 70 hadi Bilioni 3.9 kwa mwaka''.

Katika hatua nyingine Biteko amesisitiza kuwa, ''Ni mawe makubwa pekee ambayo yamepatikana kwa mara ya kwanza tangu historia ya kuchimbwa kwa Tanzanite, tukiangalia katika rekodi za serikali hakuna jiwe kubwa lenye kilo zaidi ya tano ambalo limewahi kupatikana''.

Amepongeza pia ubora wa kipindi hicho kwa kusema, ''Nashukuru kwa namna mnavyoendesha kipindi chenu haswa kwenye kipengere cha #Lenzi ni kipindi ambacho msikilizaji akianza kusikiliza inampa wakati mgumu kuiacha Radio yake niwapongeze sana timu ya Supa Breakfast''.

Jana Juni 24, 2020, mchimbaji mdogo wa madini alitangazwa kuwa Bilionea mpya nchini, mara baada ya kuchimba na kuuza mawe mawili ya madini ya Tanzanite yenye jumla ya uzito wa Kilogramu 15 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 7.8.

Post a Comment

0 Comments