tangazo

Uchaguzi wa urais Malawi: Chombo cha habari cha serikali kinasema upinzani unaongoza

Kiongozi wa chama cha Malawi Congress (MCP) Lazarus Chakwera ndiye kinara wa muungano wa upinzani
Upinzani nchini Malawi unaelekea kupata ushindi katika kura ya uchaguzi wa urais inayofanyiwa marudio baada ya matokeo yake kufutiliwa mbali kufuatia madai mengi ya udanganyifu.
Matokeo rasmi ya uchaguzi huo uliofanyika siku ya Jumanne hayajatangazwa na tume ya uchaguzi ya Malawi.
lakini chombo cha habari cha serikali MBC kinasema kwamba kiongozi wa upinzani Lazarus Chakwera anaongoza na asilimia 59 ya kura zilizohesabiwa.
Rais Peter Mutharika , ambaye anawania muhula wa pili ana asilimia 38 ya kura zilizohesabiwa, kinasema.
Mgombea wa tatu ambaye hakuonekana kama mgombea mkuu Peter Kuwani anasemekana kujiapatia asilimia 2 ya kura hizo.
Mwaka uliopita, Malawi ilikuwa nchi ya pili barani Afrika kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais kufuatia madai ya udanganyifu, baada ya Kenya 2017.
Mwandishi wa BBC katika eneo la kusini mwa Afrika, Andrew Harding anasema sio jambo la kawaida na kwa wengi linavutia - Mahakama iliingilia kati na kubadilisha matokeo katika eneo ambalo wizi wa kura ni suala la nyeti.

Muongozo wa uchaguzi wa Malawi

Wafuasi wa bwana Chakwera tayari wameanza kusherehekea kile wanachoamini ni ushindi wa kihistoria - katika kile kinachoaminika kuwa tukio la kwanza katika eneo la sahara kwamba uchaguzi uliokumbwa na udanganyifu umebadilishwa na upinzani kuibuka na ushindi ukichukua madaraka kwa njia ya kidemokrasia.
Pongezi pia zimetolewa na viongozi wa upinzani katika mataifa ya Afrika ya kusini.
"Maisha mapya kwa Malawi!," alisema kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Nelson Chamisa.
"Mungu ameipatia Malawi Mcha Mungu'', aliongezea akitaja historia ya Chakwera kama kiongozi wa dini.
''Ndugu yangu, rafiki yangu na kiongozi ameshinda uchaguzi wa Malawi. Niliwasiliana naye kwa simu na kusherehekea ushindi wake'', alituma ujumbe wa twitter kiongozi wa zamani wa chama cha upinzani cha DA Mmusi Maimane.

Subira iliojaa wasiwasi

Mwandishi wa BBC anasema taasisi za kidemokrasia nchini Malawi huenda zikakabiliwa na shinikizo kali katika saa chache na siku zijazo.
Taifa hilo lilikuwa limegawanyika kabla ya uchaguzi huo wa marudio huku kukiwa na maandamano makubwa ya kupinga serikali.
Kiongozi mkuu wa serikali amedaiwa kusema kwamba uchaguzi unaibiwa.
Watu walipiga kura Jumanne lich aya hofu ya coronavirus
Maelezo ya picha,
Watu walipiga kura Jumanne lich aya hofu ya coronavirus
Akizungumza siku ya Jumanne baada ya kupiga kura kusini mwa Malawi, bwana Mutharika alidai kumekuwa na ghasia katika maeneo ya upinzani, kilisema chombo cha habari cha Reuters.
''Inasikitisha. katibu wetu mkuu amepigwa . wale wanaosababisha ghasia hawana la kufanya '', Reuters ilimnukuu rais akisema.
''Ni vipi sasa kwamba uchaguzi huu utakuwa wa haki na huru''?, aliuliza.
Hatahaivyo ripoti hizo hazijathibitishwa.
Peter Mutharika na Lazarus Chakwera
Maelezo ya picha,
Lazarus Chakwera (Kulia) anampinga rais Peter Mutharika (Kushoto)
Akipiga kura yake kiongozi wa upinzani Chakwera alisema kwamba ana imani na tume ya uchaguzi kufanya kile kilicho cha haki.
''Naamini kwamba hatua ya raia wa Malawi kutafuta haki inajibiwa hii leo. Na naamini haki yao itaheshimiwa'', aliongezea.
Yeyote yule atakayeibuka mshindi atalazimika kupona mgawanyiko uliotokea pamoja na kukabiliana na masuala muhimu ya ufisadi, umasikini na ukosefu wa ajira.

Kwanini kulikuwa na uchaguzi?

Kura ya marudio ya uchaguzi wa Mei 2019 iliagizwa na mahakama ya kikatiba nchini Malawi mwezi Februari baada ya majaji kubaini udanganyifu mwingi.
Uchaguzi huo ulimfanya rais Mutharika kupata ushindi mwembamba wa kura 159,000 ambazo ni asilimia 38.6 ya kura zilizopigwa . Bwana Chakwera alikuwa wa pili na asilimia 35.4.
Bwana Chakwera na mgombea aliyekuwa katika nafasi ya tatu walihoji kwamba uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki.
Malalamishi yao yalishirikisha madai kwamba nakala za kuhesabu kura hizo zilifutwa na kuongezewa idadi ya kura kwa kutumia wino wa kusahihisha makosa.
Hali ya switafahamu kuhusu matokeo hayo ilizua miezi kadhaa ya wasiwasi na maandamano, yaliobadilika na kuwa ghasia kati ya wafuasi wa upinzani na maafisa wa polisi kote nchini.
Uamuzi wa mwezi februari wa kufuta matokeo hayo ya uchaguzi uliwafanya watu kusherehekea , lakini bwana Mutharika alitaja uamuzi huo kama'' mabadiliko ambayo yanaadhimisha mwanzo wa mwisho wa demokrasia nchini humo.
Mwezi uliopita, mwenyekiti wa zamani wa tume ya uchaguzi nchini Malawi Jane Ansah alijiuzulu kufuatia miezi kadhaa ya shinikizo ya waandamanaji ambao walimkosoa kwa jinsi alivyosimamia uchaguzi huo.
Kura mpya inajiri wakati ambapo kuna hofu kubwa kati ya serikali na mahakama za taifa hilo.
Pia kumekuwa na wasiwasi kuhusu mkakati na usalama wa kufanya uchaguzi katikati ya mlipuko wa virusi vya corona.

Post a Comment

0 Comments