Wanawake 1,000 wa UWT wilaya ya Dodoma Mjini wajitokeza kumdhamini Rais Magufuli

WANAWAKE wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Dodoma Mjini leo wamejitokeza kwa wingi kumdhamini Rais Dk John Magufuli katika fomu yake ya kuwania Urais kupitia chama hiko.

Zoezi hilo la ujazaji fomu limeongozwa na Katibu wa UWT Wilaya ya Dodoma Mjini, Diana Madukwa katika uwanja wa Jamhuri ambapo jumla ya wanawake 1,000 wamejitokeza kumdhamini Rais Magufuli.

Katibu huyo wa UWT Dodoma Mjini, Diana Madukwa amesema amefurahishwa na namna ambavyo akina mama hao wamejitokeza kwa wingi leo kujaza fomu za kumdhamini mgombea wao licha ya wengi wao kutoka nje ya mji.

"  Zoezi hili ni endelevu nimefurahi sana kuona wanawake wamejitokeza, waliojitokeza ni wanachama wa UWT 1,000 ambao wote wamekuja kwa lengo moja tu la kumdhamini Ndugu Magufuli ili aweze kugombea tena Urais kwa kipindi kingine cha pili.


Nitoe rai kwa wanachama wote wa UWT Dodoma Mjini na maeneo mengine nchini kuendelea kujitokeza kwa wingi kujaza fomu hizi za kumdhamini Rais Magufuli," Amesema Diana Madukwa.

Kwa upande wake Mjumbe wa kamati ya utekelezaji ya wilaya ya Dodoma Mjini (UWT), Joyce George amesema kwa upande wa akina mama Rais Magufuli amewasaidia kwa kiasi kikubwa hasa katika upatikanaji wa mikopo huku Joyna Godilisious Makewa akisema mambo makubwa yaliyofanywa na Rais ndio yamechangia wingi huo wa akina mama katika kumdhamini.

" Nani ambaye hajui kazi kubwa iliyofanywa na Rais Dk Magufuli nchini? Kila mahali maendeleo yanaonekana, sisi akina Mama hatutoishia hapa tu kwenye kumdhamini bali hata kampeni tutampigia," Amesema Joyna Makena.

Post a Comment

0 Comments