tangazo

DC Mfune apokea msaada wa vitakasa mikono na barakoa kutoka TALGWU Mkoa wa Mbeya

KATIKA kuunga mkono jitihada za serikali za kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa Corona, Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Mkoani Mbeya (TALGWU) wametoa misaada ya vifaa kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Ruben Mfune.

Vifaa vilivyotolewa na Chama hicho ni pamoja na Kipima joto, Vitakasa mikono Lita 10, Vidonge vya Klorini 500 na Barakoa zipatazo 150, huku wakiwaomba wadau wengine kujitokeza kuchangia vifaa hivyo.

Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo, DC Mfune amewashukuru TALGWU kwa kujitoa kwao katika mapambano hayo huku akiahidi kuvigawa vifaa hivyo kwenye maeneo yanayopokea watu wengi.

" Huu ni moyo wa ajabu sana ndugu zangu, niwapongeze kwa namna mlivyoguswa na mkaona ni vema kutoa mchango wenu kwenye mapambano haya ya ugonjwa huu wa Corona. Huu ndio uzalendo ambao Rais Dk John Magufuli amekua akiuhimiza. Tuendelee kuungana na kushirikiana pamoja.

Niwasihi wadau wengine, vyama mbalimbali na mashirika kuguswa kama TALGWU walivyoguswa na kushirikiana kwa pamoja katika kudhibiti maambukizi haya, siyo lazima kwa kutoa vifaa lakini hata kutoa elimu kwa wananchi wetu ya namna ya kujikinga na maambukizi ni msaada mkubwa pia," Amesema DC Mfune.

Kwa upande wake Katibu wa Chama hicho Mkoa wa Mbeya, Frank Mattio ameipongeza serikali kwa namna ambavyo imekua ikipambana na corona toka ugonjwa huo uingie nchini na kuahidi kuendelea kushirikiana na serikali katika mapambano ya ugonjwa huo kwa kuchangia vifaa na pia kutoa elimu kwa wananchi ya kujikinga na maambukizi.

" Hapana shaka kwamba Rais Dk John Magufuli ameonesha uwezo mkubwa katika jambo hili, ameruhusu watu waendelee kufanya kazi na zaidi ahadi yake juzi wakati akimuapisha Dk Mwiguli Nchemba kuwa Waziri wa Sheria na Katiba ambapo alituhakikishia Wafanyakazi wote kuwa tutaendelea kulipwa mishahara na stahiki zetu kama kawaida.

Hili ni jukumu letu sote kama Taifa. Hatupaswi kuiachia serikali ipambane yenyewe, uzalendo ni pamoja na kuungana kama Nchi kwenye mambo kama haya, tuwaombe wadau wengine wajitokeze kuiunga mkono serikali na ninaamini kwa pamoja tunaweza kuzuia na kudhibiti maambukizi ya Corona, " Amesema Mattio.

Post a Comment

0 Comments