Wakuu wa vyuo kupanga na Wizara ya Elimu mikakati kufikia malengo


Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewakutanisha Wakuu wa Vyuo Vikuu vyote  nchini  kwa lengo la kuweka mkakati wa pamoja wa namna ya kufikia malengo ya ufundishaji na ukamilishaji wa Mitaala pindi Vyuo vitakapofunguliwa Juni 1, 2020.

Akifungua kikao hicho Katibu Mkuu wa Wizara Ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo amesema pamoja na mambo mengine  watakubaliana namna bora ya kuhakikisha vyuo vinafidia muda wa masomo uliopotea na kukamilisha mihula bila kuathiri taaluma.

Mengine yaliyojadiliwa katika  kikao hicho ni kuhakikisha vyuo vinawasilisha nyaraka zote muhimu ili wanafunzi wapate Mikopo yao mapema vyuo vitakapofunguliwa.

"Hakikisheni katika vyuo vyenu  mnachagua maafisa mikopo ambao watatoa ushirikiano mzuri kwa wanafunzi ili kusiwe na malalamiko wakati wa kushughulikia mikopo yao," alisisitiza Dkt. Akwilapo.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Makamu Wakuu wa Vyuo, Marasi na Maprovosti Tanzania (CVCPT) ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Raphael Chibunda amesema wanaishukuru Wizara kwa kuitisha kikao hicho ili kuweka mipango kwa pamoja utakaowasaidia kufungua vyuo bila changamoto na kwamba vyuo tayari vimejipanga  kuhakisha Jumuiya za Vyuo zinakuwa salama dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona kwa kuzingatia  maelekezo ya wataalamu wa afya huku wakiendelea na masomo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Abdul-Razaq Badru amesema Bodi imejipanga kutoa mikopo kwa wanafunzi kwa wakati kwa kushirikiana na vyuo huku akivishauri vyuo hivyo kushirikiana na uongozi wa wanafunzi wakati wa zoezi la utoaji mikopo ili kurahisisha utekelezaji wa kazi hiyo.

Post a Comment

0 Comments