tangazo

Virusi ya Corona: Arsenal yaanza mazoezi binafsi huku mipango ya kumaliza msimu ikipamba moto

Mipango ya kuendelea na msimu wa Ligi ya Premia inatarajiwa kushika kasi wiki hii.
Mpango huo maalumu unaanza kwa Arsenal, Grighton na West Ham kufungua viwanja vyao vya mazoezi leo Jumatatu kwa wachezaji kuanza mazoezi binafsi ya kujifua.
Ligi ya Primia inatarajiwa kurejea dimbani ifikapo Juni 8 na kufikia tamatimwishoni mwa Mwezi Julai ili kuendana na mipango ya UEFA kwa mashindano ya klabu ya bara Ulaya.
Hivyo mazoezi kamili nay a kasi yanatazamiwa kuanza kufikia Mei 18.
Klabu zinazoshiriki EPL zinatarajiwa kukutana Ijumaa ili kujadili zaidi mipango ya lini watarudi uwanjani.
Ligi ya hiyo imesimamishwa tangu Machi 13 kutokana na janga la virusi vya corona na klabu zote zimedhamiria kumaliza jumla ya michezo 92 iliyosalia.
Mechi zote zinatarajiwa kuchezwa kwenye viwanja bila mashabiki, huku baadhi zikirushwa bure kwenye runinga.
Uwanja wa ArsenalHaki miliki ya pichaISABEL INFANTES
Image captionUwanja wa Arsenal
Suala moja ambalo linataraji kujadiliwa Ijumaa ni viwanja gani vitakavyoidhinishwa kutumika na idadi yake kwa ujumla.
Hata hivyo kurejea kwa ligi hiyo kunategemeana na majaribio matano ambayo yamewekwa na serikali ya Uingereza hususani kuongeza kasi ya upimaji wa watu, na kuchukua hatua za watu kujitenga.
Pia itategemea na hitimisho la litakalofikiwa na madaktari waandamizi wa michezo ambao wanatarajiwa kuja na kanuni za kiafya za kufuatwa kwa mechi zisizo na mashabiki. Madaktari haoo wanatarajiwa kuanza kukutana wiki hii pia.
BBC iliripoti Jumamosi kuwa serikali ya Uingereza inapanga kufanyika kwa mikutano hiyo ili kusaidia michezo mikubwa kurejea.
Mpango huo ulibainishwa na chanzo kilichopo karibu na mijadala hiyo kama "kuongeza kasi" ya kusaidia michezo kurejea "ndani ya wiki chache", endapo hatua chanya zitapigwa.
Zaidi ya watu 20,000 nchini Uingereza wameaga dunia kwasababu ya virusi vya corona.
Vile wachezaji wa Arsenal watakavyofanya mazoezi
Wachezaji watawasili kwa makundi ya wachezaji 5 kufanya mazoezi ya mtu mmoja mmoja, kunyoosha viungo na kukimbia na mpira
Viwanja 10 vinatumika kwa hiyo wachezaji hawatatangamana miongoni mwao
Kila mchezaji atakuwa na mpira wake
Wachezaji wamepangiwa orodha na wanaarifiwa mahala pa kuegesha magari yao
Majengo katika eneo la kufanyia mazoezi yamefungwa
Klabu hiyo inahisi kwamba kufanyia mazoezi eneo la Colney ni salama zaidi kuliko kwenye bustani, ambapo huwa wanaombwa na mashabiki wao kupiga picha nao
Jumapili, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Dominic Raab amesema itakuwa kwa vilabu vidogo kurejea msimu huu kwasababu ya kiwango cha mawasiliano lakini michezo ya kulipwa huenda ikarejea kutokana na kuimarika kwa shughuli ya upimaji ambako huenda ikaanzishwa.
Vilabu vya ligi ya Bundesliga nchini Ujerumani tayari vimeanza tena kufanya mazoezi wakiwa tayari kuanza tena msimu uliokatizwa Mei 9 iwapo wwataruhusiwa na serikali.
Nchini Italia, ligi ya Seria inaweza kuanza tena mazoezi ya mtu mmoja mmoja Mei 4 pamoja na mazoezi ya timu nzima kwa ujumla Mei 18 baada ya waziri mkuu wa Italia kutangaza hatua ya kwanza ya kulegeza masharti ya amri ya kusalia ndani kwasababu ya virusi vya corona.
Chama cha wacheza soka wa kulipwa cha kimataifa (Fifpro) kinasema kuanza tena kwa mpira wa soka kuna hatari ya kuonesha ishara mbaya.
"Kuna maswali mengi ya kimatibabu, vifaa na kisayansi kuhusu watu kufanyiwa vipimo na itifaki lakini pia ni suala la kijamii," amesema katibu mkuu Jonas Baer-Hoffmann.
"Tunahitaji mwongozo na itifaki kuhusu namna ya kurejea inayohakikisha usalama na afya njema. Mpira wa soka ni mchezo wa kutangamana na tunahisi kwamba kujilinda kwa hali ya juu kunahitajika.
"Je tunatuma ujumbe stahiki kwa jamii, na je tunahamasisha watu kurejea katika hali iliyo imara hadi maisha yatakaporejea kuwa ya kawaida? Ama pengine tunakuwa mfano mbaya na kuonesha kwamba soka ina sheria tofauti kwa ulimwengu?"

Post a Comment

0 Comments