tangazo

Utata ubunge wa Mwambe

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai ameacha maswali baada ya kusema barua ya Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika iliyoarifu Bunge kuhusu Cecil Mwambe kujivua uanachama wa chama hicho, haina maana wala mantiki.

Mwambaye ambaye alikuwa Mbunge wa Ndanda, Februari 15, alitangaza kujivua uanachama wa Chadema akiwa ofisi ndogo za makao makuu ya CCM Lumumba na kupokewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole.

Hata hivyo juzi, Ndugai alisema barua ya Chadema ya kutomtambua na kutaka Bunge lisimpe stahiki kama mbunge, haina mantiki suala ambalo limeacha maswali huku Mwambe mwenyewe akisema bado anasubiri maelekezo ya Spka ili ayafanyie kazi.

Kwa pande wake, Mnyika amesema ni vyema kwanza Spika aseme Mwambe atarejea bungeni kama mbunge wa chama gani ilihali mwenyewe ametangaza kujiengua Chadema.

Akizungumza bungeni juzi, Spika Ndugai alisema; “nimepokea barua ya Bwana John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema akimwandikia katibu wa Bunge. Kwenye barua hii anasema kwamba tusimtambue mheshimiwa Cecil Mwambe kama mbunge na asipate stahiki zozote.

“Lakini barua yenyewe jinsi alivyoiandika ni fupi, niwasomee tu. Anasema; “Bwana Cecil Mwambe alikuwa mbunge wa jimbo la Ndanda aliyekuwa amedhaminiwa na Chadema hata hivyo Februari mwaka huu alitangaza kupitia vyombo vya habari kwamba amehama chama hicho.

“Hivyo basi kwa mujibu ibara ya 7 (1 F ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekoma kuwa mbunge na ameacha kiti chake katika Bunge, kwa hiyo Bunge lisiendelee kumpatia sitahiki zozote.”

Ndugai alisema; “sasa namshangaa Mnyika kwa sababu hayo maneno anayosema alipaswa aambatanishe na barua ya Mwambe inayothibitisha haya anayosema, hakuambatanisha.

“Pili, mimi sina barua ya Mwambe ya kusema kwamba kaacha ubunge kwa hiyari yake mwenyewe, na kama ni chama hiki (Chadema) kimechukua hatua, sina viambatanisho vinavyoonyesha vikao halali vilivyofanya maamuzi hayo, kwahiyo hii barua haina maana, haina mantiki.

“Nichukue nafasi hii kuwaambia wabunge wote ‘including’ wabunge wa Chadema na wengine wanaotishwatishwa huko msibabaike, msiwe na wasiwasi, mnaye Spika imara atawalinda mwanzo mwisho, habari ya ukandamizaji na ubabaishaji hauna nafasi, fanyeni kazi zenu kwa kujiamini, mmeaminiwa na wananchi, fanyeni kazi zenu wala msiwe na wasiwasi.”

Jana akizungumza na MTANZANIA, Mwambe alisema hakusikia moja kwa moja wakati Spika akieleza kuhusu kutoitambua barua kutoka kwa Mnyika na kwamba hata hivyo alipata taarifa baadaye.

Alisema kwa sasa anaendelea kufuatilia na kuwasiliana na Ofisi ya Spika Ndugai kupata taarifa kwa usahihi na kwamba maelekezo na uamuzi wa Spika ndio utakaompa nafasi ya kuamua nini cha kufanya kwa sasa.

Mwambe alisema kwa kuwa Spika ndiye mkuu wa mhimili wa Bunge, anaendelea kusubiri maelekezo yake kuhusu nini anachohitaji kwake.

Alipoulizwa iwapo atatakiwa kurejea bungeni kwa kuwa inaonekana Ofisi ya Spika bado inatambua ubunge wake baada ya kukataa barua hiyo ya Mnyika, atarejea bungeni kwa chama gani, alijibu kwa ufupi: “Katika hilo ninasubiri maelekezo ya Spika.”

Alisema kuhusu suala la yeye kuandika barua kwa Spika baada ya kutangaza kujivua uanachama Chadema, au kuandika barua rasmi kwa chama chake cha awali, alisema hilo ni suala binafsi sana, lakini tayari alishatekeleza wajibu wake kikatiba na mengine hawezi kuyazungumia kwa undani kwa sasa.

“Kwa kweli katika hili ni suala binafsi sana, kwa upande wangu nilishatekeleza wajibu wangu wa kikatiba. Kwa sasa ninaendelea na shughuli zangu. Kwamba kama nitarudi bungeni nitarudi vipi, katika hilo nasubiri maelekezo ya Spika,” alisema Mwambe.

Post a Comment

0 Comments