tangazo

Waandamanaji wenye silaha marekani wapinga zuio la corona

Waandamanaji ambao wanapinga sheria za kubakia nyumbani ili kuzuia kuenea ugonjwa wa COVID-19 au corona wamejitokeza mitaani nchini Marekani wakiwa wamejizatiti kwa silaha tayari kukabiliana na polisi.

Maandamano hayo yanajiri wakati hasira za wananchi zikiwa zinapanda kote Marekani kutokana na sera za uchumi ambazo zimepelekea mamilioni ya Wamarekani kupoteza ajira kufuatia janga la corona.

Maandamano makubwa yameripotiwa katika jimbo la New York, ambalo linaongoza kwa vifo vinavyotokana na corona Marekani. Maandamano mengine pia yameripotiwa katika majimbo mengine zaidi ya 10 kote Marekani.

Mjini Los Angeles, wachuuzi waliandamana Mei Mosi wakisema hawawezi kupata msaada wa wasiokuwa na ajira kwa sababu kazi zao si rasmi au kwa sababu hawana vibali rasmi vya kuishi Marekani.

Katika jimbo la Michigan waandamamanaji waliokuwa na hasira walijitokeza wakiwa wamebeba silaha wakipinga hatua ya gavana wa jimbo hilo ya kuongeza muda wa kutotoka nje ili kuzuia kuenea corona.

Wiki iliyopita wafanyakazi milioni 3.8 ambao wamepoteza ajira waliwasilisha rasmi maombi ya kupata ruzuku ya wasiokuwa na ajira.
Karibu watu milioni 30.3 wamefutwa kazi kote Marekani katika kipindi cha wiki sita zilizopita baada ya kuibuka janga la corona ambalo limewalazimu waajiri kufunga kazi zao.

Hadi kufikia jana Mei pili, watu milioni 1.13 walikuwa wameambukziwa corona nchini Marekani huku waliofariki wakikaribia 66,000 na hivyo kuifanya nchi hiyo kuwa iliyoathirika vibaya zaidi na corona duniani.

Post a Comment

0 Comments