tangazo

Iran yatoa kibali cha kukamatwa kwa Trump

Serikali ya Iran imetoa ombi kwa shirika la uchunguzi la kimataifa lnterpol kutaka rais wa Marekani Donald Trump akamatwe pamoja na maelfu ya watu wanaoaminiwa kupanga njama ya kumuua mkuu wake wa majeshi Qassem Soleimani Januari mwaka huu.
Jenerali Qassem Soleimani alikuwa kiongozi wa kikosi maalum cha jeshi la Iran (Quds), ambaye aliuawa mapema mwaka huu kwa kutumia makombora yaliyodondoshwa na ndege isiyokuwa na rubani ya Marekani katika uwanja wa ndege wa Baghdad nchini Iraq.
Mkuu wa mashitaka ya umma mjini Tehran Ali Alqasimehr alisema Jumatatu kuwa Trump na watu wengine 35 waliohusika katika mauaji ya Qassem Soleimani "washitakiwe kwa mauaji na ugaidi," na kwamba shirika la uchunguzi la kimataifa (lnterpol) limeombwa kutoa usaidizi wa kukamatwa kwa watu hao, ilisema taarifa iliyotolewa na idara yake.

mgogoro wa Marekani na Iran
Idara ya ulinzi ya Marekani ilidai kumuua jeneral Qassem Soleimani kama hatua ya kujilinda.
Alqasimehr hakuwataja watu wengine wowote ambao anataka wachukuliwe hatua kando na Trump, lakini amesisitiza kuwa Iran itaendelea kufuatilia suala hilo hata baada ya kipindi chake cha urais kukamilika.
Baada ya kupokea ombi kama hilo, Interpol hushauriana ili kutathmini ikiwa itatoa maelezo au la na nchi wanachama. Interpol hata hivyo haiwajibiki kuweka wazi uchunguzi japo wakati mwingine huchapisha baadhi ya matokeo ya uchunguzi inayofanya katika mtandao wake.
Hata hivyo, Interpol imesema haitatimiza ombi la Iran.
Awali, wachambuzi wa mambo walitilia shaka ikiwa shirika hilo litaitikia ombi la Iran kwasababu muongozo wake wa kazi hauruhusu "kuingilia kati masuala ya kisiasa" ama yale yanayoegemea uhasama wa kisiasa
Wawakilishi wa Marekani kwa Iran wamesema kuwa kibali hicho ni propaganda na hakuna anayeweza kuchukulia hatua hiyo kwa uzito.
Soleimani aliuawa katika shambulio la angani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad kutokana na agizo la Trump, ambaye alisema jenerali huyo alihusika kwa mauaji ya mamia ya vikosi vya Marekani na alikuwa anakaribia kutekeleza mashambulizi mengine.
Iran ilijibu shambulio hilo kwa kurusha makombora katika kambi za kijeshi za Iraqi za wanajeshi wa Marekani.

soleimani
"Takriban watu 36 wametambuliwa kuhusishwa na mauaji ya Hajj Qasem. Walisimamia, wakachukua hatua na kuagiza kutekelezwa kwa mauaji hayo," Bwana Alqasimehr alinukuliwa na gazeti la Mehr news.
"Hilo ni pamoja na maafisa wa kisiasa na kijeshi kutoka Marekani pamoja na nchi zingine na mahakama imetoa kibali cha kukamatwa."
Bwana Trump alikuwa wa kwanza kwenye orodha hiyo na kukamatwa kwake ni jambo litakaloendelezwa hata baada ya kumaliza uongozi wake kama rais, mwendesha mashtaka amesema.
"Iran haitasitisha juhudi zake hadi watu hawa watakapo kamatwa na haki kupatikana," amesema naibu Waziri wa Mambo ya Nje Mohsen Baharvand

An Iranian holds up a picture of Qasem Soleimani in Tehran, Iran, on 4 January 2020

Maelezo ya picha,
Qasem Soleimani aliuawa kwa shambulio la anga lililoagizwa na Donald Trump

Kwa nini kuna mvutano?

Mgogoro ambao baina ya nchi hizo mbili ulianza tangu mwaka 2018 wakati rais Trump alipojitoa katika mkataba wa kimataifa wa mwaka 2015 uliolenga kumaliza mpango wa nyuklia nchini Iran.
Bw. Trump alihoji makubaliano na kusema yana kasoro, na hatimaye kuamua kuweka vikwazo.
Iran kwa upande wake iliamua kuacha kutekeleza kile ambacho iliahidi kufanya mapema mwaka 2018 na kutishia kuanza tena kutengeneza zana za nyukilia.
Kumekuwa na mashambulizi dhidi ya meli ya mizigo na mafuta katika eneo la ghuba ya Omani, ambapo Marekani na Saudi Arabia zinaishutumu Iran kuyatekeleza.
Iran hata hivyo inakanusha.
Tayari Marekani imeshaongeza uwepo wa majeshi yake na vifaa vya kivita katika eneo hilo la Mashariki ya Kati, hali inayoonesha kuwa mzozo huo si wa kuisha leo au kesho.
Mfumo wa kuzalisha nguvu za umeme kwa kutumia nguvu za nyuklia hutumiwa na mataifa mengi, Iran iliadhibiwa na kuwekewa vikwazo vya kufanya biashara na mataifa mengine baada ya kushukiwa huenda mpango wake wa nyuklia unatumiwa kuunda bomu kisiri.
Iran inasisitiza kuwa shughuli zake za kinyuklia ni salama- jamii ya kimataifa haijafanikiwa kuthibitisha kama hilo ni kweli au la.
Kati ya mwaka 2012 na 2016, Iran ilipoteza takriban pauni bilioni 118 baada ya kuwekewa vikwazo.


Bofya Hapa kusoma Habari Zingenezo

Post a Comment

0 Comments