Asilimia 40 ya wananchi wa Nigeria wanaishi katika umasikini

Takwimu zinaonyesha kuwa, asilimia 40 ya wananchi wa Nigeria yenye utajiri mkubwa wa mafuta wanaishi katika umasikini.

Shirika la Taifa la Takwimu la Nigeria limesema hayo katika ripoti yake iliyotolewa jana Jumatatu na kubainisha kwamba, ukosefu wa huduma za afya ni changamoto nyingine inayoikabili jamii ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Taarifa ya Shirika la Taifa la Takwimu la Nigeria inaeleza kuwa, watu milioni 82.9 nchini humo wanaishi katika umasikini. Hii ni kusema kuwa, watu wanne katika kila watu 10 nchini Nigeria wanaishi chini ya mstari wa umasikini


Asilimia 40 ya wananchi wa Nigeria wanaishi chini ya mstari wa umasikini nchini Nigeria ambapo wana kipato cha Naira 137,430 sawa na dola 381.75 kwa mwaka, imesisitiza taarifa hiyo hiyo.

Kiwango hicho cha umasikini kinaripotiwa nchini Nigeria katika hali ambayo, nchi hiyo ni ya kwanza barani Afrika kwa utajiri wa mafuta ikifuatiwa na Angola.

Ongezeko la idadi ya watu nchini Nigeria ambalo haliendani na kasi ya ukuaji wa uchumi pamoja na sera mbovu za serikali za kushindwa kutumia vizuri rasilimali na utajiri uliopo nchini humo ni mambo yanayoelezwa na wataalamu wa mambo kuwa, yamechangia kuongezeka umasikini nchini humo.

Imeelezwa kuwa, takwimu hizo hazijalihusisha jimbo la Borno ambalo kwa muongo mmoja sasa linakabiliwa na hali mbaya baada ya wanamgambo wa Boko Haram kuanzisha harakati zao, kwani maeneo mengi ya jimbo hilo ni vigumu kuyafikia kutokana na ukosefu wa usalama.

Post a Comment

0 Comments