Nabii Joshua ashauri Watanzania kufanya maombi "Uponyaji umekaribia kwa Taifa"

KIONGOZI Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Joshua Aram Mwantyala amewataka Watanzania kuendelea kujinyenyekeza kwa Mungu kwa kuwa Mungu anaenda kuachilia uponyaji kwa Taifa muda wowote.

Nabii Joshua amesema Mungu ni msikivu na mwaminifu kwa kila amwaminiye, hivyo kilichobakia ni Watanzania wote kuendelea kumpigia magoti na kumweleza yanayotukabili kwa sasa.

Wito huo ameutoa Yespa, Kihonda mjini Morogoro muda mfupi baada ya kuongoza maombi mfululizo ya kuliombea Taifa ili Mungu akaliponye dhidi ya virusi vya corona na changamoto mbalimbali linalokabiliana nazo kwa sasa.

Pia Nabii Joshua amemuomba Mungu azidi kuwapa viongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiongozwa na Rais Dkt. John Magufuli, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais, Samia Suluhu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na viongozi wengine moyo wa ujasiri na afya njema ili wazidi kuwatumikia Watanzania kwa moyo wa upendo.

"Ukisoma Bibilia Takatifu kitabu cha 2Mambo ya Nyakati 1:14 inaeleza kwa kina kuwa, ikiwa watu wangu, walioittwa kwa jina langu watajinyenyekeza, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni na kuwasamehe dhambi zao, na kuiponya nchi yao;

"Katika hiki kitabu cha Mambo ya Nyakati tumeona namna ambavyo ukuu wa Mungu una nguvu ya kubadili kilichoonekana hakiwezekani, kuwezekana, kubadili mateso kuwa furaha, kuiponya nchi kutoka katika magonjwa mbalimbali kama maambukizi ya virusi vya homa kali ya mapafu ya corona (COVID-19) na mengine mengi, ninaamini upnyaji unaenda kutokea muda wowote kwa taifa letu,"amesema Nabii Joshua.

Mbali na hayo amesema, kila Mtanzania katika kipindi hiki ambacho wanaendelea kumomba Mungu aendelee kuzingatia miongozo na kanuni zinazotolewa mara kwa mara na Serikali juu ya namna ya kujikinga na virusi hivyo.

"Tuzingatie sana miongozo inayotolewa na Serikali ikiwemo matumizi sahihi ya uvaaji barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni ikiwemo kutakasa mikono kwa vitakasa mikono,hizo ni silaha za vita dhidi ya Corona,"ameongeza Nabii Joshua.

Hata hivyo, Nabii Joshua amesema, huduma yake inaendelea na maombi mfululizo ikiwemo kwenda katika mlima wa Bwana kwa ajili ya kumweleza mahitaji ya Watanzania ili akapate kuwabariki kila mmoja kwa wakati wake.

Post a Comment

0 Comments