WHO: Utengezaji wa chanjo ya corona utachukua muda wa miezi 16

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) amesema, kirusi cha corona kinasambaa kwa wingi na kinaua sana na akaongeza kuwa, utengezaji wa chanjo ya kinga ya kirusi hicho unahitaji muda wa miezi 10 hadi 16.

Tedros Adhanom ameyasema hayo katika kikao cha Baraza la Kiuchumi-Kijamii la Umoja wa Mataifa kilichofanyika kwa njia ya mawasiliano ya intaneti na kwa anuani ya "Sera athirifu za kukabiliana na Covid-19".

Adhanom amesema, hadi sasa watu karibu milioni nne wameripotiwa kwa WHO kuwa wamekumbwa na ugonjwa wa Covid-19 na akabainisha kuwa, juhudi zinazofanywa kwa ajili ya kutengeza chanjo ya corona zilianza tangu mwezi Januari lakini unahitajika muda wa miezi 10 hadi 16 mpaka kufikia mafanikio kamili.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani ametilia mkazo pia udharura wa kudhaminiwa bajeti ya fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi wa utengezaji chanjo ya corona na akaeleza kwamba, dola bilioni nane zilizoahidiwa kuchangiwa na nchi za Ulaya hivi karibuni kwa ajili ya mradi wa chanjo hiyo hazitoshi.


Matamshi ya Mkurugenzi Mkuu huyo wa shirika muhimu zaidi la kimataifa lenye jukumu la kupanga na kuratibu vita vya kupambana na maradhi ya maambukizo hususan Covid-19 yametolewa huku serikali ya Marekani inayoongozwa na Donald Trump ikiwa imeamua kukata bajeti ya fedha inayochangia kwa ajili ya shirika hilo ili kuficha udhaifu wake wa kushindwa kukabiliana ipasavyo na janga la corona nchini humo.

Washington imedai kuwa WHO inaipendelea China na kwamba haikuweza kuzipatia nchi taarifa zinazohitajika katika hatua za awali za kuzuka mripuko wa corona.

 Takwimu za karibuni zinaonyesha kuwa, watu wasiopungua 4,137, 591 wameambukizwa maradhi thakili ya Covid-19 yanayosababishwa na kirusi cha corona duniani kote na hadi sasa watu 283,526 wameshaaga dunia kutokana na maradhi hayo


ADVERTISEMENT

Post a Comment

0 Comments