tangazo

Changamoto ambazo hazikwepeki kwa mjasiriamali yeyote yule

Labda unawaza kuhusu kujikita katika ujasiriamali katika muda huu. Pengine tayari wewe ni mjasiriamali tayari mwenye biashara moja au zaidi. Leo tutaangalia changamoto unazoweza kukutana nazo kama mjasiriamali ili uweze kujiandaa vizuri kuzishinda pale utapokutana nazo.

Changamoto ya kukubali kuachana na mshahara
Kwa wengi mshahara unafanya uepuke mawazo ya shida za kipesa kwa sababu unajua kuwa kila tarehe flani nitapata kiasi flani. Ni hali ambayo inaweza kuzoeleka kirahisi sana na kumfanya mtu aogope kuuacha pale atapoamua kujiingiza katika ujasiriamali kwa muda wote. Inabidi ujiandae na hili toka siku ya kwanza unayoanza ujasiriamali.

Changamoto ya kusimamia mtaji
Jinsi unavyotumia mtaji wako kunaweza kufanya biashara yako ifanikiwe au ishindwe. Iwapo utatumia mtaji kwa matumizi yasio ya lazima basi mtaji wako utaisha haraka na kuna uwezekano mkubwa biashara yako haitadumu zaidi ya miezi sita,Kufanya maamuzi sahihi ya katika utumiji wa  mtaji wako utavyokutana na vitu vya ziada vinavyohitajika ofisini kutakufanya ufanikiwe.

Kusimamia ishu za Biashara
Hapo juu nimeongelea kuhusu kusimamia mtaji ila kuna mambo mengine mengi yanaweza kutokea katika biashara yako. Vitu kama mmoja wa wafanyakazi wako kuchelewa kazini mara kwa mara, au labda benki kufungwa kabla ya wewe kukamilisha muamala muhimu na hata kukuta kuwa bidhaa zinakudodea wakati ulidhani zitauzika haraka. Kuna ishu nyingi sana za kibiashara ambazo zinaweza kukuletea changamoto. Jinsi utavyosimamia mambo katika changamoto hizi aidha kutakufanya ufanikiwe au usifanikiwe.

Upweke
upweke ni moja kati ya vitu ambavyo utakutana navyo katika safari yako kuelekea mafanikio na pengine hata utapofanikiwa. Itafika siku utakuta mambo hayaendi unavyotaka na huna wa kumpigia kumlalamikia. Unaweza usiweze kutafuta ndugu na marafiki kwa sababu walikuambia usijiingize katika ujasiriamali.

Pia katika siku nyingi utajikuta upo ofisini peke yako mpaka usiku wa manane kukiwa hamna mtu wa kukuletea hata kahawa kukuzuia usilale. Hakuna kuchekacheka na watoto, kuteta na marafiki ama kujiliwaza na mama watoto. Ni wewe na kazi tu. Ni vema ukajua hili mapema kwa sababu kwa wengi jambo hili huwafanya wakate tamaa,usikate tamaa na ukifanya jitihada utatimiza malengo yako.

Changamoto ya kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja 
kwa mjasiriamali unayeanza, kuna kipindi itabidi uwe unahusika kutenda vitu vingi katika biashara yako. Wewe unaweza ukawa ndie unauza vitu dukani kwako. Wewe huyohuyo unaweza ukawa ndie unaepost bidhaa zako katika Instagram. Wewe huyohuyo unaweza ukawa ndie unaepokea simu zote zinazoingia katika biashara yako.

Kabla hujaanza kuajiri watu wakusaidie basi utakuwa na majukumu mengi.
Changamoto inakuja kwenye jinsi ya kuyafanyia kazi majukumu hayo vizuri ili biashara yako iendelee kukua. Na hapa ndipo umuhimu wa kuwa tayari kujifunza unapoingia. Hutajua kila kitu hivyo ni vema ukajitahidi kutafuta wale wanaojua vitu flani wakufundishe. Yote haya ni muhimu ili kuhakikisha unafanikiwa.

Kukabiliana na mfumo wa maisha
Iwapo wewe ratiba yako ya wikiendi ni ya viwanja basi ukishaanza ujasiriamali hili litabadilika. Kuna watu ratiba zao ni kuwa Alhamisi ni kuzuka Ladies Night club, Ijumaa na Jumamosi disco kisha Jumapili mchana hadi saa 4 usiku kijiweni na washkaji wakipata moja moto moja baridi huku wakipiga soga za hapa na pale. Hata kama huyu sio wewe kwa asilimia mia moja, ni vema ukatambua kuwa utapoanza ujasiriamali basi muda wako mwingi utatumika katika biashara yako na si kwenye starehe. Itabidi uanze kukataa mialiko ya kwenda kula bata na washkaji. Itabidi matumizi yako ya pesa yaelekee katika kuikuza biashara yako na si kwingineko.

Na pia mara nyingi itabidi ubadilishe kabisa marafiki zako uwe na wale ambao hawatakurudisha nyuma katika safari yako ya ujasiriamali. 
Na hapa ndipo wengi wanapogonga mwamba. Wao wanataka mafanikio katika ujasiriamali huku wakiendelea na starehe. Ukweli ni kwamba hakuna aliyefika mafanikio makubwa kwa namna hiyo. Hivyo ni vema ukafanya maamuzi ya nini unataka katika maisha yako iwe bata au mafanikio katika ujasiriamali. Iwapo ni ujasiriamali basi jiandae kubadilisha mfumo wako wa maisha ili ufikie mafanikio.

ADVERTISEMENT

Post a Comment

0 Comments