tangazo

TFF: Mazoezi ya pamoja hayaruhusiwi

Shirikisho la soka nchini TFF, limezitahadharisha klabu za soka zinazoshiriki madaraja mbalimbali kutoanza mazoezi ya pamoja hadi Serikali itakapotoa tamko rasmi.

TFF wametoa tahadhari hiyo licha ya Serikali kusema bado inaendelea na mchakato wa kurejesha Ligi Kuu ya Tanzania Bara kufuatia tamko la Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk John Pombe Joseph Magufuli.

TFF imesema mchakato huo bado ni wa ndani, hivyo wanachama wake wote wanapaswa kuendelea kutekeleza agizo la awali la Serikali la kuepuka mkusanyiko kwa maana ya kutoanza maozezi ya pamoja hadi hapo maelekezo mengine yatakapotolewa.

wishoni mwa juma lililopita Rais Magufuli wakati akimuapisha Waziri mpya wa Katiba na Sheria, Dk. Mwigulu Nchemba wilayani Chato mkoani Geita, alisema kwamba anafikiria kuruhusu Ligi Kuu iendelee kwa sababu hajasikia mwanamichezo hata mmoja ameathiriwa na virusi vya Corona.

Pia Bodi ya Ligi (TPLB) jana jumanne ilikuwa ina kikao na Kamati ya Tiba ya TFF kupata ushauri wa kitaalamu juu ya namna Ligi itakavyoendeshwa kwa kuzingatia tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona, vinavyosababisha ugonjwa wa COVID19.

Kamati ya Tiba ipo chini ya Mwenyekiti, Dk. Paul Marealle, Makamu wake, Dk. Fred Limbanga na Wajumbe Dk. Norman Sabuni, Dk. Lisobina Kisongo, Dk. Eliezer Ndama, Dk. Billy Haonga, na Dk. Violet Lupondo.

“Pamoja na michakato ya ndani ya TFF na TPLB kuhusu mashindano yake kuendelea, bado hatima ya kurudi kwa mashindano yote itategemea uamuzi wa Serikali, ambayo itaelekeza muda mwafaka wa kurejea kwa mashindano,”.

TFF ilisimamisha ligi zake zote Machi 17, mwaka huu ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatia mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa corona duniani kote.

Pia TFF ilivunja kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars iliyokuwa inajiandaa na fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zilizopangwa kuanza Aprili 4 hadi 25, mwaka huu nchini Cameroon ambazo pia zimeahirishwa kwa sababu ya COVID 19.

Kwa ujumla CAF ilisimamisha mechi zote za kufuzu za mashindano ya Afrika kwa ushauri wa Shirika la Afya Dunani (WHO) kufuatia mlipuko wa virusi vya corona hadi hapo itakapaoamuliwa vinginevyo.

Ligi Kuu ilisimama huku Simba SC ikiwa inaongoza kwa alama zake 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye alama 54 baada ya timu zote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Yanga SC ni wa tatu kwa alama zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na alama 50 za mechi 28.

Post a Comment

0 Comments